Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, amewasisitiza wawekezaji katika sekta ya utalii kuhakikisha miradi yao inaleta tija ya moja kwa moja kwa wananchi wa maeneo husika kupitia uzalishaji wa ajira na fursa za biashara, sambamba na kuchangia uchumi wa Zanzibar.
Agizo hilo limetolewa katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga, wakati wa uzinduzi rasmi wa hoteli mpya ya Joud by the Sea iliyopo Jambiani, Kusini Unguja, ambapo alibainisha kuwa ongezeko la uwekezaji ni dhihirisho la kuimarika kwa imani ya wawekezaji visiwani humo lakini ni lazima matokeo yake yaonekane kwa jamii inayozunguka miradi hiyo.
Akielezea mwenendo wa sekta hiyo, Dkt. Mwinyi alieleza kuwa Zanzibar ilifanikiwa kupokea watalii 917,167 mwaka 2025 ikilinganishwa na watalii 736,755 mwaka 2024, takwimu zinazoashiria kuongezeka kwa asilimia 24.5 na kuifanya Zanzibar kuwa kivutio kinachozidi kung'ara kimataifa, jambo linaloitaka serikali na sekta binafsi kuendelea kuimarisha ubora wa miundombinu, huduma na malazi ili kuendana na ushindani wa soko la utalii duniani.
Aliongeza kuwa uwekezaji katika sekta ya hoteli una uwezo mkubwa wa kufungua masoko mapya kwa bidhaa za ndani, wakulima, wajasiriamali wadogo na wa kati, huku akipongeza uongozi wa hoteli hiyo kwa kutoa ajira 85 kati ya 85 zilizopo kwa wananchi wa eneo hilo, hatua aliyoitaka iigwe na wawekezaji wengine wote.
Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amewataka wawekezaji kuzingatia matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini, kulinda mazingira, kudumisha viwango vya juu vya huduma, na kushirikiana kwa karibu na jamii, huku akiahidi kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji pamoja na miundombinu ya kimkakati kama vile barabara, viwanja vya ndege, bandari na huduma za afya.
Aliwakumbusha pia wananchi kuendelea kulinda amani na usalama ili wageni wajisikie salama, wakati akitoa pongezi kwa wawekezaji hao kutoka nchi za Kiarabu kwa kuchagua Zanzibar, pamoja na kuipongeza Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Wizara ya Kazi na Uwekezaji kwa kurahisisha utekelezaji wa mradi huo.
Naye mmiliki wa hoteli hiyo, Ahmed Baki, alieleza kuwa hoteli hiyo yenye vyumba 40 imesanifiwa kwa kuangazia utamaduni wa pwani ya Zanzibar, huku akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi ni Watanzania na Wazanzibari, na kwamba awamu ya pili ya mradi huo inatazamiwa kuongeza vyumba zaidi pamoja na kuanzisha huduma za ustawi, afya na mgahawa wa kisasa.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment