" VIONGOZI WA DINI WAKUMBUSHWA KUSIMAMIA AMANI NA MALEZI BORA YA VIJANA

VIONGOZI WA DINI WAKUMBUSHWA KUSIMAMIA AMANI NA MALEZI BORA YA VIJANA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu kuweka kipaumbele katika kuhubiri amani, upendo, umoja na mshikamano huku wakijikita katika kuimarisha malezi ya watoto na vijana kwenye misingi imara ya maadili mema.

Dk Mwinyi alitoa kauli hiyo baada ya Sala ya Ijumaa alipokuwa akifungua rasmi mkutano mkubwa wa Ijitimai ulioandaliwa na Jumuiya ya Tabligh Markaz Zanzibar katika eneo la Bungi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, tukio ambalo limewakutanisha waumini kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya siku tatu za mafundisho na dua.

Akizungumza mbele ya maelfu ya waumini waliofurika katika eneo hilo, Dk Mwinyi alisisitiza kuwa mashehe na wahadhiri wanaoshiriki wana wajibu mkubwa wa kuwakumbusha waumini mambo ya kheri na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wazuri wa yale wanayojifunza ili yaakisiwe katika maisha yao ya kila siku kwa ajili ya ustawi wa jamii.

Aliongeza kuwa wazazi, walezi na viongozi wanapaswa kuwa macho na ushawishi wa mabadiliko ya kijamii na matumizi ya mitandao ya kijamii, akibainisha kuwa pamoja na mitandao kuwa na faida za kielimu na kidini, inahitaji ufuatiliaji wa karibu ili kulinda kizazi kipya dhidi ya maudhui yasiyofaa.

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi aliwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari stahiki na kuzingatia maelekezo ya mamlaka kuhusu mvua kubwa zinazotarajiwa, sambamba na kuongeza dua za kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha taifa na majanga ya kimaumbile.

Aidha alisema serikali itaendelea kushirikiana bega kwa bega na jumuiya mbalimbali kuimarisha miundombinu, ikiwemo mpango wa kupanua barabara inayoelekea eneo hilo kuwa njia nne na kuendeleza huduma za elimu ya dini kama vile madrasa, ili kuhakikisha Zanzibar inaendelea kubaki kuwa kisiwa cha amani kinachovutia wageni na kukuza maendeleo endelevu.

Post a Comment

Previous Post Next Post