" Vyombo vya habari nchini vyasimama kidete kusaka suluhu ya taarifa potofu na matamshi ya chuki

Vyombo vya habari nchini vyasimama kidete kusaka suluhu ya taarifa potofu na matamshi ya chuki




Waandishi wa habari, wahariri, na wataalamu wa masoko kutoka taasisi kumi za habari nchini Tanzania wamejengewa uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto ya taarifa potofu, upotoshaji, na matamshi ya chuki kupitia mafunzo maalum ya Ubunifu Unaomlenga Mtumiaji yanayofanyika kwa siku tatu mfululizo jijini Arusha kuanzia Septemba tisa hadi kumi na moja, 2026.

Mafunzo haya ya kimkakati yanayoendeshwa na Shirika la International Media Support (IMS) kwa kushirikiana na Kampuni ya Teknolojia na Habari ya Nukta Africa, Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), na JamiiAfrica, yanalenga kuwezesha vyombo vya habari kuandaa mawazo na suluhu zinazozingatia mahitaji, uzoefu, na tabia halisi za wananchi wanaotumia taarifa hizo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen, amesisitiza kuwa taarifa sahihi ni rasilimali nyeti inayomwezesha mwananchi kufanya maamuzi sahihi ya maendeleo, huku akionya kuwa kuenea kwa taarifa potofu na chuki kuna uwezo mkubwa wa kuhatarisha ustawi wa jamii na kuathiri sekta mbalimbali, jambo linalowalazimu waandishi kutumia mbinu za kisasa kubaini na kuchambua maudhui hayo kupitia Programu ya Maabara ya Fikra Bunifu na Uvumbuzi.

Kwa upande wake, Programu Meneja wa IMS, Fausta Musokwa, amewakumbusha waandishi wa habari kuwa wao ni walinzi wakuu wa demokrasia ambao wanapaswa kujitofautisha na watoa taarifa wa mitandaoni kwa kuhakikisha wananchi wanapata habari zilizothibitishwa, huku akieleza kuwa kasi ya intaneti na simu janja imeongeza hatari ya usambazaji wa taarifa zisizo sahihi zinazoweza kupotosha maamuzi ya jamii.

Naye Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwanzilishi wa HCD Services Tanzania, Dkt. Hellen Maziku, amefafanua kuwa mtazamo wa Ubunifu Unaomlenga Mtumiaji unalenga kuchimbua mahitaji na matarajio ya wananchi ili kupata suluhu thabiti, wakati washiriki wenyewe wakieleza kuwa mafunzo hayo yatawapa nguvu mpya ya kuchakata taarifa kwa umakini mkubwa ili kulinda uaminifu wa vyombo vya habari na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Post a Comment

Previous Post Next Post