Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kutoruhusu maendeleo ya teknolojia kuathiri uzingatiaji wa maadili na misingi ya taaluma wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa Waandishi wa Habari wa EFM na TVE, yaliyofanyika Septemba 9 na 10, 2026 katika Ofisi za Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
“Mkiwa Waandishi wa Habari, mna wajibu wa kuhakikisha mnasimamia misingi ya taaluma kwa kuzingatia sheria, kuepuka kutoa taarifa za uongo na kujiepusha na makosa ya jinai,” amesema Wakili Kipangula.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Mkuu wa Vipindi wa EFM, Bw. Evalist Razeck, amewasihi wamiliki wa vyombo vya habari kuwapa Waandishi wa Habari fursa ya kushiriki mafunzo ya mara kwa mara ili kujikumbusha misingi muhimu ya taaluma na kuwawezesha kukusanya na kutoa taarifa zenye tija kwa jamii wanayoihudumia.
Naye Mtangazaji wa EFM, Bi. Fatuma Muhidini Likwata, amesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa kuhusu maadili na misingi ya taaluma, jambo litakalowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia maslahi ya jamii.
“Mafunzo haya yametukumbusha umuhimu wa kuzingatia maadili na misingi ya taaluma katika kila hatua ya kazi yetu, kuanzia kutafuta taarifa hadi kuzifikisha kwa jamii kwa usahihi na uwajibikaji,” amesema Bi. Likwata.
Mafunzo hayo yamejikita katika mada mbalimbali, zikiwemo Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya uandishi wa habari na uzalendo katika utangazaji.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya JAB ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari, kwa lengo la kuimarisha weledi na uzingatiaji wa maadili na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment