" Zaidi ya Vijana 4,200 Wanufaika na Ajira Nchi za Kiarabu

Zaidi ya Vijana 4,200 Wanufaika na Ajira Nchi za Kiarabu



Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikishirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimefungua milango ya ajira katika nchi za Kiarabu na kufanikisha kunufaisha vijana 4,211 kati ya mwaka 2025 hadi 2026.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mtambile, Alley Masoud Alley, aliyetaka kujua idadi ya vijana waliopata nafasi za kazi nje ya nchi kupitia makubaliano yaliyopo.

Waziri Sharif amefafanua kuwa kati ya ajira hizo, 3,527 ni kwa ajili ya wanawake, huku nafasi 684 zikiwa ni za wanaume zilizopatikana katika nchi kama vile Qatar, Oman, na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ameongeza kuwa nafasi hizo zinapatikana kwa kuratibiwa na mawakala walioingia mikataba na taasisi za nchi husika, huku serikali ikiweka taratibu thabiti ikiwemo utoaji wa viza na ushirikishwaji wa balozi za Tanzania nje ya nchi ili kuondoa usumbufu, changamoto, na matukio ya udhalilishaji yaliyokuwa yakijitokeza hapo awali.

Aidha, amebainisha kuwa wizara yake inashirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutoa mgawanyo sawa wa nafasi hizo, hatua ambayo imeondoa kabisa malalamiko na mivutano ya zamani ambapo Zanzibar ilikuwa haipati mgao stahiki wa ajira za nje.

Post a Comment

Previous Post Next Post