" WANANCHI SHINYANGA WAFIKISHA CHANGAMOTO ZA KIUSALAMA KWA KAMANDA MAGOMI

WANANCHI SHINYANGA WAFIKISHA CHANGAMOTO ZA KIUSALAMA KWA KAMANDA MAGOMI

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga wamewasilisha changamoto mbalimbali za kiusalama kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, ikiwa ni pamoja na changamoto ya upatikanaji wa leseni za udereva na baadhi ya madereva wa pikipiki kuendesha kwa fujo.

Changamoto hizo zimewasilishwa leo Oktoba 8, 2026, katika Stendi ndogo ya Soko Kuu ndani ya Manispaa ya Shinyanga, kupitia kampeni ya Jeshi la Polisi ya “Ongea na Kamanda”, inayolenga kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kusikiliza changamoto mbalimbali za kiusalama zinazowakabili.

Baadhi ya madereva wameeleza changamoto wanazokutana nazo katika kupata leseni kutokana na masharti ya kisheria, huku wakiomba kuwepo kwa vyuo vilivyosajiliwa vinavyoweza kutoa mafunzo ya muda mfupi na kuwapatia vyeti vinavyoweza kuwasaidia kukidhi masharti ya kupata leseni.

Kwa upande mwingine, wananchi wamelalamikia baadhi ya madereva wa pikipiki wanaoendesha kwa fujo na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.Akijibu changamoto hiyo, Kamanda Magomi amesema Jeshi la Polisi litazungumza na madereva hao kesho ili kuwapa maelekezo yanayostahili, huku akieleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakidai kuwa na vibali ambavyo, kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa, hawana.

Aidha, wananchi wamewasilisha malalamiko kuhusu baadhi ya watu wanaojihusisha na matukio ya utapeli, ambapo Kamanda Magomi aliahidi kufuatilia suala hilo kwa ukaribu na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Wananchi hao pia wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kutenga muda wa kuwasikiliza moja kwa moja na kutoa fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.

Kampeni ya “Ongea na Kamanda” ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi kuwafikia wananchi katika maeneo yao, kusikiliza changamoto za kiusalama na kuzitafutia ufumbuzi. Kwa Mkoa wa Shinyanga, kampeni hiyo imeendelea leo ikiwa ni siku yake ya pili.

 

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post