Diwani wa
Kata ya Ndembezi ambaye pia ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya
Shinyanga, Pendo Sawa, ameilalamikia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) kwa kutowashirikisha viongozi wa kata na mitaa kabla ya kuanza kwa
shughuli za ujenzi wa barabara, akieleza kuwa hali hiyo imesababisha ajali
iliyogharimu maisha ya mkazi mmoja wa kata hiyo.
Pendo
ameyasema hayo katika mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa
ya Shinyanga uliojadili taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali kutoka
katika kata za manispaa hiyo.
Amesema
mkandarasi anayetekeleza kazi katika eneo la barabara inayopita karibu na Shule
ya Balina alianza kazi bila kutoa taarifa kwa viongozi wa eneo husika, huku
akimwaga vifusi katika maeneo ambayo viongozi wa mtaa na kata
hawakushirikishwa, hali iliyosababisha hatari kwa watumiaji wa barabara.
Amesema kwa
bahati mbaya, vifusi hivyo vilisababisha ajali iliyomhusisha mkazi wa Kata ya
Ndembezi, aliyeumia vibaya na baadaye kufariki dunia, huku mazishi yake
yakifanyika siku moja kabla ya mkutano huo.
Akijibu hoja
hiyo, mwakilishi wa TARURA, Victoria Pamba, amesema walifika katika eneo la
ajali na kwamba tayari wamempa mkandarasi maelekezo kuhusu suala hilo.
Ameahidi
kuwa mkandarasi atafika kwa Diwani wa Kata ya Ndembezi kwa ajili ya
kujitambulisha na kuhakikisha utekelezaji wa kazi unaendelea kwa ushirikiano na
viongozi wa eneo hilo.
Post a Comment