Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya (Mb), ameendelea na ziara yake mkoani Iringa kwa lengo la kukagua hali ya uwekezaji, kuhamasisha uwekezaji wa ndani, kuhamasisha Mikoa na Halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha kongani za viwanda na pia kusikiliza changamoto za wawekezaji na kutolea ufafanuzi.
Akiwa Mkoani humo, Mhe. Dkt Chaya ametembelea Kiwanda cha kuchakata maziwa cha ASAS ambacho kimewekeza mtaji jumla ya bilioni 600.
Akizungumza katika kiwanda hicho Mhe. Dkt. Chaya amesema kampuni ya ASAS kimefanya uwekezaji mkubwa na kutoa ajira kwa vijana hivyo Serikali ina jukumu la kuwalea.
Mhe. Dkt.Chaya amesema kuwa amezichukua changamoto mbalimbal zilizotolewa ikiwemo upungufu wa malighafi , ubora wa maziwa yanayokusanywa, katika kulitatua hilo Mhe. Dkt Chaya amesema Ofisi watashirikiana na Wizara ya mifugo na uvuvi kuwasaidia wafugaji wadogo na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta ya mifugo na kuja na mbegu za kisasa ambazo zitazalisha maziwa ya kutosha
Amebainisha kuwa Serikali itashughulikia suala la kodi waliloliwasilisha. “ Mhe. Rais hataki kuona mwekezaji anafunga uwekezaji , ndio maana tuna kuja huku kuwafuatilia , kusikia changamoto zao na kutafuta utatuzi wa changamoto hizo”.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Isimani, Mhe. Emanuela Mtatifikolo (Mb), amepongeza uwekezaji wa ASAS Dairies, akieleza kuwa kiwanda hicho kina mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya maziwa, kukuza kipato cha wafugaji na kutoa ajira kwa wananchi. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa maziwa ili kukidhi mahitaji ya viwanda.
Naye Mkurugenzi wa ASAS , Bw. Ahmed Salim Asas amesema kiwanda hicho kimewekeza zaidi ya bilioni 600 na kina uwezo uwezo wa kuchakata lita 300,000 za maziwa kwa siku, lakini kwa sasa kinachakata lita 100,000 pekee kutokana na uhaba wa malighafi. Maziwa hayo yanatoka kwenye mashamba ya kampuni na kwa wazalishaji wadogo kupitia vituo 20 vya kukusanyia maziwa vilivyopo Iringa na Mbeya. Kiwanda pia kinaajiri takribani wafanyakazi zaidi ya 400.
Aidha, mwekezaji ameeleza changamoto zinazokikabili kiwanda kuwa ni gharama za uzalishaji na usafirishaji, kiwango kidogo cha unywaji wa maziwa nchini, ubora wa maziwa na changamoto za kikodi .
Bw Salum Assas amebainisha kuwa kiwanda kinaendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa mashuleni kupitia programu inayohudumia shule 40, pamoja na kushirikiana na maafisa ugani kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu uzalishaji wa maziwa bora.
Post a Comment