" TAKUKURU YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 106 KATIKA STESHENI YA SGR MOROGORO

TAKUKURU YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 106 KATIKA STESHENI YA SGR MOROGORO

 

NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 106.08 zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya ununuzi na usafirishaji wa maji kwa magari maalumu (bowser) katika Stesheni ya Reli ya Kisasa ya Jakaya Kikwete kwa mwaka mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro Casius Kiaro, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya taasisi hiyo kubaini changamoto ya upatikanaji wa maji katika kituo hicho kupitia ufuatiliaji wa huduma za kijamii.

Amesema ufuatiliaji huo ulihusisha Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) pamoja na uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), kwa lengo la kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

Ameeleza kuwa kabla ya hatua hiyo, Stesheni ya SGR ya Jakaya Kikwete haikuwa na huduma ya uhakika ya maji, hali iliyolazimu kituo hicho kununua na kusafirisha maji kwa kutumia magari maalumu kwa ajili ya matumizi ya kawaida pamoja na huduma za mabehewa ya treni.

Kwa mujibu wa Kiaro, gharama za ununuzi na usafirishaji wa maji zilifikia zaidi ya shilingi milioni mbili kwa wiki, sawa na shilingi milioni 8.84 kwa mwezi na jumla ya shilingi milioni 106.08 kwa mwaka.

“Kupitia ushirikiano huo, huduma ya maji safi na salama imeanza kupatikana kwa uhakika katika kituo hicho kuanzia mwezi Agosti 2026, hatua iliyopunguza utegemezi wa ununuzi wa maji kwa kutumia magari,” amesema Kiaro.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Stesheni ya Jakaya Kikwete, Salvatory Kimaro, amekiri kuwa changamoto ya upatikanaji wa maji ilikuwa ya muda mrefu, lakini imekwisha baada ya TAKUKURU kufuatilia suala hilo na kuwakutanisha na MORUWASA ili kupata suluhisho.

Kimaro amesema kwa sasa kituo hicho kinapata maji saa 24, ingawa bado kuna uhitaji wa kuboresha miundombinu ya kuhifadhi maji ili kuwa na akiba ya kutosha kwa matumizi ya kituo hicho.

“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TRC, napenda kuishukuru sana TAKUKURU kwa hatua hii. Tulikuwa tunapata shida kubwa ya maji na kutumia gharama nyingi kununua na kusafirisha maji kwa ajili ya matumizi ya kituo,” amesema Kimaro.

Naye Meneja wa Kanda Namba Moja wa MORUWASA, Mhandisi Gidion Chahe, amesema pamoja na kutatua changamoto hiyo, mamlaka hiyo inaendelea na mikakati ya kuboresha miundombinu ya maji ili kuhakikisha kituo hicho kinapata huduma ya uhakika kulingana na ongezeko la matumizi ya maji linalotokana na kuongezeka kwa idadi ya abiria.

Amesema maboresho hayo ni muhimu ili kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kupatikana kwa uhakika hata kadri shughuli za usafiri wa reli zinavyoendelea kukua.

Hata hivyo, TAKUKURU imeeleza itaendelea kufanya ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo zinatumika ipasavyo na miradi inayotekelezwa inazingatia thamani

Post a Comment

Previous Post Next Post