
Na Sophia Kingimali Dar es Salaam.
TANZANIA imepata fursa ya kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi baada ya kusaini makubaliano na Sekretarieti ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ya kuwa mwenyeji wa mikutano ya kimataifa, hatua itakayoiwezesha nchi kuandaa mikutano miwili kuanzia Februari 2027.
Hatua hiyo ni miongoni mwa matokeo ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 31 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) uliofanyika Antalya, Uturuki, ambapo pia nchi imepata ahadi za kifedha na fursa za uwekezaji zenye thamani ya takribani Dola za Marekani bilioni 4.7 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kimazingira.
Akitoa taarifa ya matokeo na manufaa ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Mhandisi Hamad Masauni amesema fursa hiyo ya kuwa mwenyeji wa mikutano ya UNFCCC inatarajiwa kuimarisha diplomasia ya tabianchi na kukuza utalii wa mikutano nchini.
Amesema pamoja na fursa hiyo, Tanzania imepata ahadi ya Dola milioni 54 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kununua majiko 70,000 ya kisasa yanayotumia umeme kwa shule na vituo vya afya, pamoja na Dola milioni 26 kwa ajili ya kuhifadhi mifumo ikolojia ya pwani na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.
Aidha, Serikali ya Uingereza kupitia UK Aid imeahidi Pauni milioni nne, ambapo Pauni milioni mbili zitaelekezwa katika nishati safi ya kupikia na nyingine milioni mbili katika nishati jadidifu, huku ikisaidia wananchi milioni moja kupata majiko ya umeme kupitia utaratibu wa kulipia gharama kidogo kidogo kwenye bili za umeme.
Masauni amesema taasisi ya SEforALL imeahidi kuijumuisha Tanzania katika uwekezaji wa zaidi ya Dola bilioni nne wa nishati safi ya kupikia, huku kampuni ya UpEnergy ikiahidi kuendeleza mradi wa nishati hiyo katika shule 3,000 za umma wenye thamani ya Dola milioni 30 kupitia ushirikiano wa Tanzania na Japan katika biashara ya kaboni.
Ameongeza kuwa Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi umeahidi kuidhinisha miradi yenye thamani ya Dola milioni 40 kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), huku Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Kijani (GCF) ukiahidi Dola milioni sita kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa Tanzania kuandaa miradi ya kukabiliana na athari za tabianchi.
Kwa upande mwingine, Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu umeidhinisha mchakato wa kupata Dola milioni 20 kupitia CRDB Bank kwa ajili ya kusaidia jamii za visiwa vidogo, maeneo ya pwani na kanda za maziwa, hususan Pemba, Unguja, Kigoma na Pwani.
Katika hatua nyingine,Mhandisi Masauni amesema Tanzania imeimarisha uwezo wake wa kunufaika na fedha za kimataifa baada ya GCF kutoa ithibati kwa NEMC, na kuifanya nchi kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika zenye taasisi mbili zilizoidhinishwa kupata fedha za mfuko huo, ambazo ni NEMC na CRDB Bank. Pia, Ofisi ya Makamu wa Rais imesaini makubaliano na taasisi za IETA, Evercity UG na Verra kwa ajili ya kuimarisha usimamizi na biashara ya kaboni.
Masauni amesema mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa Kituo cha Vijana Wajadili wa Tabianchi Afrika (Youth Negotiators Centre), kitakachojenga uwezo wa vijana kushiriki katika majadiliano ya kimataifa, pamoja na Zanzibar kutambuliwa kuwa Jiji Linalosimamia Taka Vizuri (Zero Waste City) na kuchaguliwa katika maeneo 20 ya awali duniani kutekeleza mpango wa maeneo yasiyo na taka. Alisema Serikali itafuatilia ahadi na fursa zote zilizopatikana ili kuhakikisha zinageuzwa kuwa miradi na manufaa halisi kwa wananchi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
PROFESSOR MGOKO EPISODE 08
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment