" WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA AHITIMISHA ZIARA YAKE MKOANI SHINYANGA, ATOA MAELEKEZO SEKTA MBALIMBALI

WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA AHITIMISHA ZIARA YAKE MKOANI SHINYANGA, ATOA MAELEKEZO SEKTA MBALIMBALI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Shinyanga kwa kutoa maelekezo mbalimbali yanayolenga kutatua changamoto za wananchi katika sekta za afya, elimu, barabara, maji, kilimo, nishati na madini.

Dkt. Mwigulu amehitimisha ziara hiyo leo Novemba 11, 2026, kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Segese, Jimbo la Msalala, Wilaya ya Kahama, baada ya kuanza ziara hiyo Novemba 8, 2026, katika Wilaya ya Kishapu.

Katika kipindi cha siku nne, Waziri Mkuu ametembelea Halmashauri sita za Mkoa wa Shinyanga ambazo ni Kishapu, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Manispaa ya Shinyanga, Manispaa ya Kahama, Ushetu na Msalala, huku akifanya pia mkutano na wananchi wa Jimbo la Itwangi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amekutana na wananchi katika mikutano ya hadhara, kupokea hoja na malalamiko yao na kutoa maelekezo kwa viongozi na watendaji wa Serikali kuhusu hatua za kuchukua ili kutatua changamoto zilizowasilishwa.

Miongoni mwa maelekezo aliyoyatoa ni pamoja na kuimarisha huduma za afya, ambapo alisisitiza wagonjwa wa dharura na wajawazito kuhudumiwa bila kucheleweshwa kwa sababu za kiutawala. Pia alielekeza kutokuwepo kwa utaratibu wa kuwachangisha wagonjwa fedha za mafuta ya magari ya wagonjwa, huku akitaka fedha hizo zitengwe katika bajeti za vituo na mamlaka za afya.

Aidha, alielekeza uchunguzi wa changamoto ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wagonjwa kuelekezwa kununua dawa katika maduka binafsi licha ya taarifa za vituo kuonyesha dawa zimepokelewa.

Katika sekta ya elimu, Dkt. Mwigulu aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanamaliza masomo yao na kutowaruhusu kuacha shule kwa ajili ya kwenda kufanya shughuli za uchimbaji madini. Ametoa msisitizo huo katika mkutano wa mwisho wa ziara hiyo Msalala, akieleza kuwa elimu itawasaidia watoto kuwa na fursa za maisha hata pale shughuli za uchimbaji madini zitakapopungua au kumalizika.

Pia akiwa Jimbo la Itwangi, Waziri Mkuu alitoa maelekezo kuhusu ajira kwa walimu wawili wa kujitolea wa Shule ya Msingi Masunula, baada ya shule hiyo kushika nafasi ya pili kitaifa katika matokeo ya darasa la saba. Aliagiza hatua za kuwaajiri walimu hao zifuatiliwe kupitia mamlaka husika.

Katika sekta ya miundombinu, Waziri Mkuu alielekeza TANROADS kuharakisha usanifu wa kina wa barabara ya Ushetu–Kahama ili iweze kuzingatiwa katika maandalizi ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha. Pia alitoa maelekezo ya kukamilisha usanifu na maandalizi ya kitaalamu ya barabara za kipaumbele katika maeneo ya Msalala, Ushetu na Kishapu, kwa lengo la kuziwezesha kuingia katika hatua za utekelezaji.

Akiwa Msalala, alipokea ombi la kujenga barabara zinazounganisha maeneo ya uzalishaji na miundombinu muhimu ya usafirishaji, ikiwemo eneo la Isaka. Alieleza umuhimu wa kuipa kipaumbele miundombinu inayorahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.

Kuhusu sekta ya kilimo, Waziri Mkuu aliwaelekeza Mawaziri wenye dhamana ya TAMISEMI, Fedha na Kilimo kupitia upya muundo wa tozo zinazohusiana na pembejeo, hususan kwa wakulima wa tumbaku, baada ya Mbunge wa Ushetu kuwasilisha changamoto ya gharama za mikopo na tozo zinazoongeza mzigo kwa wakulima.

Pia alieleza kuwa katika msimu ujao wa zao la pamba, Serikali inalenga kuwepo kwa wanunuzi wengi badala ya mfumo wa mnunuzi mmoja ili kuongeza ushindani na kuwanufaisha wakulima.

Katika sekta ya nishati, Dkt. Mwigulu alieleza kuwa Serikali inaendelea na mradi mkubwa wa kuimarisha Gridi ya Taifa ili kukabiliana na changamoto ya kukatika kwa umeme inayochangiwa na ongezeko la matumizi. Alielekeza pia TANESCO kuendelea kuwaunganishia umeme wananchi kwa gharama ya Shilingi 27,000 katika maeneo yanayostahili.

Kwa upande wa sekta ya madini, aliwataka maafisa madini kuhakikisha masilahi ya wananchi wenye maeneo yanayopatikana madini yanazingatiwa, ili wenye mashamba, wenye leseni na wawekezaji waweze kunufaika na shughuli za uchimbaji.

Aidha, alipokea ombi la kuanzishwa kwa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Halmashauri ya Msalala itakayotoa mafunzo yanayohusiana na madini, akieleza kuwa Serikali italifanyia kazi ombi hilo.

Katika masuala ya utawala na huduma za kijamii, Waziri Mkuu alipokea ombi la wananchi wa Itwangi la kutaka eneo hilo kuwa Halmashauri inayojitegemea na kuelekeza kukamilishwa kwa huduma na miundombinu ya msingi ili kufikia vigezo vinavyohitajika. Pia alielekeza maandalizi ya ujenzi wa vituo viwili vya afya katika Kata za Usule na Didia, pamoja na kutafuta Shilingi milioni 76 za kukamilisha Zahanati ya Mwamkanga.

Akizungumzia usimamizi wa miradi ya maendeleo, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa fedha zinazotolewa na Serikali lazima zionekane katika kazi zilizokusudiwa, akitaka miradi ikamilishwe kwa wakati na kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha zilizotumika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameahidi kuwa mkoa utaendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu, kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wa taasisi mbalimbali ili changamoto zilizowasilishwa zipatiwe ufumbuzi.

Mhe. Mhita pia ameeleza kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, Mkoa wa Shinyanga umepokea jumla ya Shilingi trilioni 2.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya, elimu, maji, barabara na nishati.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amesema chama hicho kinaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kupitia Serikali yake, huku akiwapongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutekeleza ahadi na mipango ya maendeleo iliyoainishwa katika Ilani ya uchaguzi.

Waziri Mkuu amehitimisha ziara yake kwa kusikiliza hoja za wananchi wa Msalala na kutoa maelekezo kwa viongozi na watendaji wa Serikali, huku akisisitiza kuwa changamoto zilizowasilishwa hazipaswi kubaki kwenye mikutano bali zinapaswa kufanyiwa kazi na kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Msalala katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Segese, Wilaya ya Kahama, Novemba 11, 2026, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Shinyanga.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post