Askofu
wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kesho Jumanne
tarehe 28.03.2023, ataweka wakfu Mafuta ya Krisma takatifu, pamoja na kubariki
mafuta ya wagonjwa na Wakatekumeni.
Misa
ya Krisma ambayo itaanza saa 4:00 asubuhi, itafanyika katika Kanisa kuu la Mama
mwenye Huruma Ngokolo mjini Shimyanga, na itahudhuriwa na Mapadre kutoka katika
Parokia zote za Jimbo, pamoja na waamini.
Kupitia
Misa hiyo, Mapadre wote watarudia viapo vyao vya kipadre mbele ya Askofu wa
Jimbo, na baadaye waamini watapata nafasi ya kuwapongeza kwa majitoleo
waliyoyafanya kupitia huduma za kiroho walizowapatia, katika kipindi cha mwaka
mzima.
Mafuta
ya Krisma ambayo huwekwa Wakfu na Askofu wa Jimbo mbele ya Mapadre na waamini
siku chache kabla ya adhimisho la Pasaka, hutumiwa na Kanisa kwa ajili ya
kutakatifuza wakati wa utoaji wa Sakramenti mbalimbali za Kanisa, ambazo ni
pamoja na Ubatizo, Kipaimara na Sakramenti ya Daraja (Ushemasi, Upadre na
Uaskofu)
Mafuta
hayo pia hutumika kutakatifuza vifaa mbalimbali vinavyotumika kwa kazi za ibada
na Misa takatifu, ikiwemo Kanisa, Altare na Kalisi.
Kwa
upande wa mafuta ya wagonjwa, wanapakwa ili kuwatia neema maalum, kuwapa nguvu
na kuwafariji katika ugonjwa wao, pamoja na kuwaandaa kwa ajili ya kukutana na
Mwenyezi Mungu.
Aidha,
mafuta ya Wakatekumeni hupakwa wanafunzi wa dini kabla ya kupewa Sakramenti ya
ubatizo, ili kuwaimarisha katika mapambano ya kiroho yanayodaiwa katika maisha
ya Kikristo.
Post a Comment