" ASKOFU SANGU AHIMIZA WAKRISTO KUMRUDIA MUNGU ILI ASAMEHE DHABI

ASKOFU SANGU AHIMIZA WAKRISTO KUMRUDIA MUNGU ILI ASAMEHE DHABI

 Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, limeungana na Kanisa zima kote ulimwenguni kuadhimisha kilele cha hija ya huruma ya Mungu, kupitia Misa takatifu ambayo imefanyika katika kituo cha hija ya Huruma ya Mungu kijimbo kilichopo Kanisa la Mtakatifu Petro Mtume Parokia ya Nkololo Wilayani Bariadi mkoa wa Simiyu.

Katika mafundisho yake, Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amewataka Wakristo kumrudia mwenyezi Mungu mwenye huruma, ambaye wakati wote yuko tayari kuwasamehe dhambi zao.
Amewaasa Wakatoliki kuitangaza huruma ya Mungu kwa watu wote kuanzia ngazi ya familia, huku wakionyesha mfano kwa kuishi maisha ya toba,unyenyekevu, kusameheana na kuacha vitendo vya chuki, masengenyo na ukatili kwa watoto.
Askofu Sangu ametumia nafasi hiyo kuwaalika Waamini wote wa Jimbo la Shinyanga kuweka utaratibu wa kwenda kusali mara kwa mara kuomba huruma ya Mungu katika kituo cha hija cha Nkololo, ili kujipatanisha zaidi na mwenyezi Mungu, badala ya kusubiri kipindi cha hija pekee.
Kupitia Domika ya Huruma ya Mungu , Askofu Sangu ameahidi kuwarudisha kwenye utume Mapadre wawili wa Jimbo ifikapo Januari mwaka 2024, ambao ni Padre Philemon Shija na Vicent Masuke walioko kwenye mapumziko ya malezi.
Dominika ya Huruma ya Mungu huadhimishwa na Kanisa siku ya Jumapili ya kwanza baada ya Pasaka, ili kukumbuka jinsi Yesu Kristo alivyojifunua kupitia Mtakatifu Faustina na kutoa mwaliko wa kutambua kuwa, Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko udhaifu wa Mwanadamu na kwamba, yeyote anayeikimbilia kwa toba ya kweli ataikuta wazi kwenye mikono ya Mungu mwenye Huruma, ambaye atakuwa tayari kumpokea na kumkaribisha katika mfano wa Mwana Mpotevu .

Post a Comment

Previous Post Next Post