" ASKOFU SANGU AKEMEA WAKRISTO WANAOKIMBILIA VIONGOZI WA DINI KUPATA UTAJIRI WA MIUJIZA

ASKOFU SANGU AKEMEA WAKRISTO WANAOKIMBILIA VIONGOZI WA DINI KUPATA UTAJIRI WA MIUJIZA

Wakristo wamewatakiwa kuacha uvivu kwa kudanganyika kwamba, wanaweza kupata mafanikio na utajiri kwa njia ya kuwakimbilia viongozi wa dini ili wawapatie miujiza, na badala yake wanapaswa kuomba huku wakifanya kazi kwa bidii.

Akitoa mafundisho ya kiimani kupitia Misa ya Dominika ya Matawi, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu ameonya kuwa, pamoja na kwamba Mungu anao uwezo wa kumpa binadamu mafanikio, lakini mafanikio hayo hayaji kwa watu kukaa na kusubiri miujiza badala ya kufanya kazi.

Askofu Sangu amewataka Wakristo wote kuwa na imani thabiti isiyojaribiwa, huku akiwatahadharisha kujiepusha na wimbi la watu wanotumia neno la Mungu kuwalaghai na kuwaaminisha kuwa, wanaweza kuwapa mafanikio na utajiri ikiwemo nyumba na magari kwa njia ya miujiza bila ya kufanya kazi, ambapo wakati mwingine hutumia fursa hiyo kuwafanyia matendo yanayodhalilisha utu wao.

Katika hatua nyingine, Askofu Sangu amewakumbusha watu wenye nafasi mbalimbali katika utumishi wa umma na huduma za jamii kuzingatia misingi ya haki, ikiwa ni pamoja na kuepuka kumkosea Mwenyezi Mungu kwa kutumia nafasi walizonazo kama fursa ya kujinufaisha kupitia shida za wengine.

Ametumia nafasi hiyo kuwasihi watalaam wa afya kuwahudumia wagonjwa kwa upendo na uaminifu, kwani kwa kufanya hivyo watajiweka karibu zaidi na mwenyezi Mungu.

Askofu Sangu amewakumbusha Wakristo wote kudhihirisha imani yao ndani ya jamii kwa kudhibiti roho ya wivu na kufurahia mafanikio ya wengine pamoja na kuwa chimbuko la faraja, utulivu, matumaini na amani ndani ya jamii.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akitoa mafundisho ya kiimani kupitia Misa ya Dominika ya Matawi

 Misa ya Dominika ya Matawi ikiendelea katika Kanisa kuu la Mama mwenye Huruma Ngokolo mjini Shinyanga



Post a Comment

Previous Post Next Post