" MKOA WA KIGOMA KUWARUDISHA SHULENI WATOTO ELFU THELASINI WALIO NJE YA SHULE.

MKOA WA KIGOMA KUWARUDISHA SHULENI WATOTO ELFU THELASINI WALIO NJE YA SHULE.

Zaidi ya watoto elfu thelasini walio nje ya shule mkoani Kigoma, wanatarajiwa kurudishwa shuleni kupitia mpango wa elimu ya msingi kwa walioikosa MEMKWA, 

Hayo yamebainika wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya siku tano ya walimu wa MEMKWA, walimu wakuu na maafisaelimu wa kata tano za halmashauri ya wilaya ya Kasulu yaliyofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Ualimu Kasulu.

Akitoa taarifa ya mafunzo hayo, Afisaelimu ya Watu Wazima mkoa wa Kigoma Hawamu Tambwe amesema, mpango huo wa kuwapatia watoto elimu nje ya mfumo rasmi, utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano na kuzihusisha halmashauri zote za mkoa wa Kigoma.

Amesema kuwa katika utekelezaji wa mpango huo, jumla ya  watoto 32,564 wenye umri wa miaka 9-16 watahusika kati yao wavulana wakiwa 15,420 na wasichana 17,144.

"Kupitia mpango huo, watoto 4,959 wanatarajiwa kurudishwa shuleni mwaka wa kwanza, watoto 6,024 watarudishwa shuleni mwaka wa pili, watoto 6,408 watarudishwa shuleni mwaka wa tatu, watoto 7,165 watarudishwa shuleni mwaka wa nne huku watoto 8,008 wakitarajiwa kurudishwa shuleni katika kipindi cha mwaka wa mwisho wa mpango huo", amesema.

Tambwe ameongeza pia kuwa, mpango huo unaofadhiliwa na fedha kutoka kwa mfalme nchi za Kiarabu, ni matokeo ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alipomtembelea mfalme huyo.

Sambamba na ufadhili huo, mpango huo pia unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Rais Tamisemi, Shirika la Kimataifa la UNICEF na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia Elimu ya Watu Wazima Godliver Nkala, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha watoto walio nje ya shule, wanaingizwa katika mpango huo.

"Wapo watoto wanaotamani kupata elimu lakini hawaipati kutokana na sababu mbalimbali, tumetoa maelekezo kila mtoto ana haki ya kupata elimu hata kama hana sare, walimu wapokeeni watoto kwa upendo na myafanye mazingira ya vituo hivyo kuwa rafiki", amesema.

Ameongeza kuwa, chimbuko la takwimu za watoto walio nje ya shule, ni utafiti uliofanyika na kuibaini mikoa ya Kigoma, Songwe na Tabora kuwa na idadi kubwa ya watoto hao.  

Aidha kupitia kikao hicho, Nkala amepigilia msumari suala la chakula cha mchana shuleni kwa kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuihamasisha jamii na kushiriki kikamilifu katika kufanikisha jambo hilo.

Akifunga mafunzo hayo katibu tawala wa wilaya ya Kasulu Mughuha Titus amesema, pamoja na ufadhili uliotolewa ili kuutekeleza mpango huo, sio jambo la kujivunia kuuona mkoa wa Kigoma ukiwa na idadi kubwa ya watoto wasioenda shule.

Kupitia mafunzo hayo Mughuha amewataka viongozi wa kata na vijiji kuwasaka watoto wanaostahili kujiunga na mpango huo na kuwapeleka shule ili baada ya miaka mitano, tatizo la kuwepo kwa kundi hilo liwe historia.

Watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji kutoka katika kata tano zilizo kwenye mpango huo, walishiriki siku ya mwisho ya mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yaliyowasilishwa na Dr. Sempeho Siafu  na Oliver Kindole kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima,  yamefanyika pia kwenye mikoa ya Songwe na Tabora.

Post a Comment

Previous Post Next Post