Na Baraka Messa, Ileje
KUTOKANA na miundo ya vyoo vya wanafunzi wa madarasa ya awali darasa la kwanza katika shule ya Msingi Malangali wenye thamani ya shilingi milioni 34.5 wilayani Ileje kujengwa kwa kutozingatia ubora , Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) imeagizwa kufanya uchunguzi .
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya hiyo Farida Mgomi wakati alipokwenda kukagua ujenzi wa vyoo kwenye mradi wa Usafi wa Mazingira Maji na Afya(WASH) kwenye shule tano za msingi wilayani humo wenye thamani ya Sh193.79 milioni,
kabla ya ukaguzi huo kulikuwa na malalamiko kwa baadhi ya wananchi wakidai kuwa watoto wao hasa wa madarasa ya awali na darasa la kwanza wataendelea kukosa huduma bora kutokana na kutojengwa kwa viwango kulingana na mwongozo wa elimu.
Mgomi amesema Takukuru inatakiwa kufanya uchunguzi kwani mradi huu umebainika kutozingatia vipimo vya ramani ya ujenzi ukilinganisha na sehemu zingine ambapo vipimo ni milimita 320 lakini wao wamejenga milimita 200. Hivyo kupunguza ubora wa vyoo hivyo ambavyo ni kwa ajili ya watoto wadogo .
Mgomi amesema wilaya ya Ileje imepokea fedha Sh193.7 milioni kutoka benki ya Dunia kupitia wizara ya elimu kwa ajili ya ujenzi wa matundu 65 ya vyoo kwenye shule tano za msingi ambazo zilikuwa na vyoo vibovu na kuhatarisha afya na usalama kwa wanafunzi hasa wa madarasa ya awali na la kwanza .
"Fundi mkuu wa ujenzi wa mradi huu anasema mhandisi ndiye alimcholea ramani hii ambayo haipo kwenye mwongozo ,hivyo Takukuru hakikisheni mnafanya uchunguzi kwa kina pia ujenzi usimame mpaka pale tutakapojua Kuna makubaliano gani kati ya wasimamizi wa mradi ambao ni idara ya elimu msingi pamoja na wahandisi wa ujenzi," amesema Mgomi.
Aidha Mgomi amewataka wahandisi wa ujenzi wilayani humo kusimamia ujenzi wa miradi kwa uadilifu, kuijenga kwa viwango bila kufanya hujuma kulingana na thamani ya fedha inayotolewa na serikali.
Angomwile Pwele fundi wa ujenzi kwenye mradi wa Malangali amesema ukaguzi huo umesaidia kubaini makosa ya ramani amabyo alipewa na mhandisi wa ujenzi na kwamba maelekezo ya mkuu wa wilaya kwa Takukuru yataleta majibu ya nini kipo nyuma ya pazia.
Therezia Obeid afisa elimu watu wazima akizungumza kwaniaba ya afisa elimu msingi wilayani humo amezitaja shule zilizonufaika na mradi huo na kutatua changamoto ya matundu ya vyoo hasa kwa wanafunzi wa elimu ya awali kuwa ni Bupigu shule ya msingi Sh 34.5 milioni, Ishenta Sh 40.5 milioni, Itumba Sh 36.8 milioni, Malangali Sh 34.5 milioni na Nyerere Sh 47.5 milioni
"Shule ya msingi Bupigu vinajengwa vyoo matundu 11, Ishenta matundu 14, Itumba matunda 12, Malangali matundu 11,Nyerere matundu 17 , kukamilika kwa matundu haya kunaenda kusaidia kutatuliwa kwa changamoto ya miundo mbinu ya vyoo ," amesema Therezia.
Alisema sera ya elimu inazitaka shule zote za Msingi kuwa na madarasa mazuri ya elimu ya awali pamoja na kuwa na miundo mbinu mizuri ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi wadogo wa madarasa hayo ya awali na darasa la kwanza.
Elizabeth Mshani na Martini Kayange wakazi wa Malangali wamesema miradi mingi kwenye kata hiyo imekuwa ikikumbwa na doa baada ya kumalizika ikiwemo ya elimu, hivyo wanapongeza juhudi za Serikali kuwapa ushirikiano na kubaini kasoro zilizopo kwenye ujenzi , huku wakiitaka kuwachukulia hatua watakaobainika kukwamisha mradi huo.
Post a Comment