KWA mara ya nne katika misimu sita, Simba imeshindwa kuvuka hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulala 2-0 dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo Ijumaa usiku.
Bao la dakika ya 47 la kiungo Amr El
Soulia na penalti ya dakika 90 ya mshambuliaji Mahmoud Abdel Moneim yameifanya
Simba ing’oke kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya pia kufungwa 1-0 jijini Dar es
Salaam.
Hata hivyo, licha ya Simba kupoteza mchezo huo wa pili wa robo fainali wekundu hao walionyesha kiwango kizuri hasa kipindi cha kwanza ikimaliza dakika 45 za kwanza kwa kupiga mashuti mawili yaliyolenga lango huku wenyeji wao wakiwa hawana shuti lililolenga lango.
Mashuti hayo mawili ya Simba yalipigwa dakika ya 35 la kwanza likipigwa na mshambuliaji Said Ntibazonkiza 'Saido' kipa Mustapha Shobeir kupangua kisha mpira kurudi mchezoni na kumkuta kiungo Clatous Chama na kumwekea pasi safi Fabrice Ngoma lakini shuti lake likapanguliwa tena na kipa huyo.
BENCHIKHA MABADILIKO MADOGO
Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha
hakubadili kikosi chake lakini alibadilisha kidogo nafasi za wachezaji wake
akimuanzisha Saido kama mshambuliaji wa kati feki akipishana na Kibu Denis
ambaye alicheza nafasi hiyo kwenye mchezo wa kwanza na Ijumaa hii alipelekwa
pembeni.
Ahly walitumia upande wa beki wa kulia wa Simba kupitisha mashambulizi yao mengi ambayo yalizalisha bao la kwanza baada ya Kapombe kushindwa kumdhibiti beki wa kushoto wa Ahly, Ally Maaloul ambaye alikuwa kila wakati akipandisha mashambulizi hasa kipindi cha pili.
SIMBA KAMA YANGA
Simba imejikuta ikifanana na Yanga
kwa kuondolewa kwenye robo fainali lakini sio hilo tu timu zote zikitupwa nje
bila ya kufunga bao lolote ndani ya dakika 180 kwa kila timu.
Simba ilitawala umilika wa mpira
katika mechi hii kwa asilimia 55 dhidi ya 45 za wenyeji na katika mchezo wa
kwanza pia Simba iliachiwa kumiliki mpira halafu Ahly ikatumia mianya kushinda
mechi zote mbili.
Simba ilipoteza nafasi nyingi Dar es
Salaam na ugenini pia ilikosa utulivu mbele ya lango jambo ambalo liliathiri
matokeo ya Wanamsimbazi ambao pia wanahitaji kuwa na mshambuliaji bora baada ya
kule Cairo pia kuanza bila ya mshambuliaji asilia kutokana na kutowaamini kina
Freddy Koublan na Pa Omar Jobe.
Post a Comment