YANGA imecheza mpira mkubwa lakini
imeshindwa kuamua mechi na kujikuta ikiondolewa kwenye hatua ya robo fainali ya
Ligi ya Mabingwa Afrika mikwaju ya penalti 3-2 mbele ya Mamelodi Sundowns
nchini Afrika Kusini.
Timu ya Wananchi ilikwenda Afrika
Kusini ikiwa inahitaji kupata japo sare ya mabao baada ya mechi yao ya awali
jijini Dar es Salaam kumalizika kwa suluhu, lakini ikashindwa kupata ushindi
licha ya kutengeneza nafasi nzuri zaidi katika mechi zote mbili – zikiwamo za
wazi zaidi za Clement Mzize nchini Afrika Kusini na hata Dar es Salaam.
TATIZO NI HILI
Yanga ilipungua ukali kutokana na
kuwakosa katika mechi zote mbili nyota wao watatu muhimu wa kikosi cha kwanza
ambao ni uti wa mgongo wa timu hiyo, beki wa kulia Yao Kouassi, kiungo wa
ulinzi Khalid Aucho na kiungo wa ushambuliaji, Pacome Zouzua kutokana majeraha.
Lakini licha ya kuwakosa wakali hao,
Yanga bado ilicheza vyema kwa nidhamu ya hali ya juu katika mechi zote mbili
dhidi ya mabingwa hao wa Afrika wa kombe jipya la AFL ndani ya dakika zote 180,
ni Yanga iliyokaribia zaidi kufunga kwa shuti lile la Aziz Ki na pia ikipoteza
nafasi nyingi za wazi.
Mechi hizi mbili pia zimethibitisha
wazi ni kwanini Yanga inahitaji kumpata mshambuliaji wa kiwango cha juu baada
ya kuondoka kwa Fiston Mayele.
BASI LA YANGA
Kama kuna kitu ambacho kocha Miguel
Gamondi alifanikiwa basi ni mfumo wa kujilinda aliorudi nao kwenye mechi hiyo
ambao uliwaweka kwenye wakati mgumu Mamelodi kushindwa kuwa na mchezo rahisi
mjini Pretoria kama ilivyokuwa nyumbani Dar es Salaam.
Gamondi ambaye alianza na mfumo wa
4-4-2, vijana wake wanne wa kati walifanya kazi kubwa kufunga njia za wenyeji
kukamilisha mashambulizi yao kupitia katikati na kuwafanya Mamelodi kutumia
upande wa pembeni kumwaga mashambulizi lakini bado Yanga ilikuwa imara.
Wakati Mamelodi ikiwa kwenye nusu ya
Yanga wageni walikuwa wanajikuta wako 9-10 dhidi ya wenyeji 7-8 na kuweka ugumu
kwa Masandawana kukamilisha mashambulizi yao.
BACCA, DIARRA KAZI KUBWA
Wakati Mamelodi ikitumia njia za
pembeni kupandisha mashambulizi bado ikakutana na uzito kutoka kwa ulinzi wa
Yanga wakiongozwa na beki Ibrahim Hamad 'Bacca' ambaye alikuwa imara kucheza
mipira ya kichwa wakati kipa wake Djigui Diarra akionyesha ubora wa kucheza
krosi za wenyeji na kupoza presha ya mechi.
BAHATI YA LOMALISA
Ndani ya dakika 16 za kwanza Yanga
ilinusurika kucheza pungufu baada ya beki wake Lomalisa Mutambala kumchezea
vibaya beki Khuliso Mudau kisha kupewa kadi ya njano na mwamuzi Dahane Beida
kutoka Mauritania.
Baada ya kadi hiyo bado mwamuzi
Beida akarudishwa kulitazama tukio hilo kwa mara ya pili kwenye VAR lakini bado
Beida akasimamia uamuzi wake na Lomalisa kunusurika kadi nyekundu.
MKUDE DAH!
Kiungo Jonas Mkude ambaye alisifiwa
kwa kucheza vyema mechi ya Dar es Salaam, alikuwa imara tena akivuruga mipango
ya Masandawana, lakini kati ya makosa adimu aliyofanya katika mechi hiyo nusura
liigharimu mapema Yanga katika dakika ya 38 pale alipompasia kimakosa winga wa
Mamelodi, Thembinkosi Lorch ambaye angekuwa makini angeifunga Yanga lakini
akapoteza nafasi hiyo pale shuti lake lilipotoka nje kidogo.
YANGA BILA SHUTI 45 ZA KWANZA
Mpaka dakika 45 za kwanza
zilipomalizika Yanga ilipiga mashuti mawili wakati Mamelodi ikipiga mashuti
manne lakini ni shuti moja tu lililolenga lango lililopigwa na wenyeji huku
wageni wakiwa hawana shuti lililolenga lango.
UTATA SHUTI LA AZIZ KI
Yanga ililalamikia kunyimwa bao
katika dakika 59 pale Stephanie Aziz KI alipopiga shuti na mpira kugonga besela
kabla ya kudunda chini ukiaminika umeingia wavuni, lakini VAR ikaamua sio bao
na kuzua utata wa uhalali wa uamuzi huo kufanyika bila ya kuwepo kwa teknolojia
ya ‘goal line’.
Aziz Ki, ambaye amekuwa akihusishwa
na mipango ya kutimkia Mamelodi mwisho wa msimu huu wakati mkataba wake
utakapomalizika huku akiwa hajasaini kuuongeza wa kubaki Yanga, alipiga shuti
hilo lililozua utata baada ya kupigiana ‘one-two’ na Kennedy Musonda.
Shuti hilo lilimfanya Azizi kuanza
kuishangilia huku Mamelodi wakidai sio bao kisha VAR ikamsaidia tena refa Beida
kuamua kuwa halikuwa bao.
Yanga pia ilipoteza nafasi nyingine
dakika ya 78 kupitia mshambuliaji wake Clement Mzize aliyeingia katika dakika
ya 68 akichukua nafasi ya Musonda aliyepata maumivu pale alipopokea pasi safi
kutoka kwa Aziz Ki lakini akapiga nje akiwa hatua chache langoni.
Mpaka dakika 90 zinakamilika timu
hizo zilimaliza kwa suluhu nyingine na kuifanya mechi hiyo kwenda kuamuliwa kwa
‘matuta’ wenyeji wakishinda kwa penalti 3-2.
Kipa wa Mamelodi, Ronwen Williams,
ambaye aliokoa penalti nne katika mechi moja ya Afcon 2023 wakati akiitumikia
timu yake ya taifa ya Afrika Kusini, ameibuka shujaa kwa Mamelodi baada ya
kuokoa penalti mbili za kwanza za Yanga zilizopigwa na Aziz KI, beki Dickson
Job huku Bacca akipaisha wakati Augustine Okrah na Guede walifunga.
Mamelodi penalti zao zilifungwa na
Marcelo Allende, Lucas Ribeiro na Neo Maema wakati ile ya Leandro Sirino
ilipanguliwa na Diarra.
Kipigo hicho kimezima ndoto ya Yanga
kwenda nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika
historia yake na pia kwa mara ya kwanza tangu irejee baada ya kushindwa kufuzu
hatua ya makundi kwa miaka 25.
Post a Comment