" MWENGE WA UHURU WAZINDUA JENGO LA WAGONJWA MAHUTUTI WILAYA YA SIHA MKOANI KILIMANJARO

MWENGE WA UHURU WAZINDUA JENGO LA WAGONJWA MAHUTUTI WILAYA YA SIHA MKOANI KILIMANJARO

Na Mary Mosha, SIHA MWENGE wa Uhuru umezindua jengo la wagonjwa mahututi katika hospitali maalum ya Taifa ya magonjwa ambukizi Kibong'oto iliyogharimu Bilioni 1.282 wilayani Siha mkoani Kilimanjaro. Akisoma taarifa ya mradi huo kwa kiongozi wa mbio za Mwenge, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dkt Leonard Subi alisema kuwa, mradi huo ni matokeo ya kazi kubwa na nia thabiti ya serikali ya awamu ya sita kupitia fedha za Uviko 19 kwa maendeleo na ustawi wa Taifa. Dk Subi alisema kuwa, ukarabati wa mradi huo ulianza Januari 6 mwaka 2022 na kukamilika Juni 30 mwaka 2022 ambapo gharama zilizotumika ni pamoja na ununuzi wa vifaa tiba na mafunzo kwa wataalam. Alisema kuwa, katika fedha zilizotumika Bilioni 1.180 ni fedha za Uviko 19 kutoka serikali kuu huku milioni 102.708 ni mapato ya ndani ya hospitali. "Vifaa vilivyonunuliwa ni vitanda maalum vya wagonjwa wa ICU 10, mashine za kisasa za kusaidia mgonjwa kupumua 10, vifaa vya ufuatiliaji wa mgonjwa wakati wa matibabu 10, vifaa vya kuzindulia mfumo wa uhai unapokatika, ultrasound mpakato na tembezi, mashine za kuvuta makamasi au majimaji njia ya hewa pamoja na vifaa tiba vingine kwa wagonjwa mahututi" Alisema Dk. Subi. Mkurugenzi huyo alisema kuwa, hospitali hiyo pia ilipokea vitanda 8 na vifaa vingine kutoka kwa Bohari kuu la Dawa (MSD) kwa ajili ya ICU huku jumla ya wataalam 16 wa kada mbali mbali walipatiwa mafunzo maalum ya utumiaji wa vifaa tiba. Alisema kuwa, jengo hilo la ICU linauwezo wa kuhudumia wagonjwa mahututi 20 kwa mpigo ambapo mradi huo haukuwahi kutekelezwa tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo miaka 98 iliyopita lengo la serikali likiwa ni kusogeza huduma karibu na wananchi badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma. Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Godfrey Mzava alisema kuwa, Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameendelea kuboresha huduma za afya ambapo amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anaweka miundombinu na vifaa tiba na kuwajengea uwezo wataalam wa Afya ili kuhakikisha wanatoa huduma stahiki. Mzava alisema kuwa, Mwenge wa Uhuru unaendelea kuhamasisha mapambano dhidi ya maadui watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi na kudai kuwa hospitali ya Kibong'oto ni kubwa na ya kisasa ambayo inahudumia wagonjwa wa kifua kikuu kwa levo ya Kitaifa na kuwapongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa jinsi walivyosimamia fedha za uboresha wa jengo la wagonjwa mahututi. 

 

Post a Comment

Previous Post Next Post