Ticker

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI UVCCM WILAYA YA SHINYANGA VIJIJINI WATAKIWA KUSIKILIZA,KUPOKEA NA KUTATUA KERO ZINAZOWAKABIRI VIJANA

Na Elisha Petro, Shinyanga

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Shinyanga ndugu Benard Benson Werema ameongoza kikao cha Kamati ya Utekelezaji  Wilaya ya Shinyanga Vijijini kata ya Didia ambapo amezungumza na viongozi wa  Umoja huo Wilaya ya  Shinyanga Vijijjini na kuwataka kuwa karibu zaidi na vijana ili kubaini na kutatua kero mbalimbali  zinazowakabiri.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mwenyekiti Benard amewataka viongozi kuepuka kutumia muda mwingi kujipambanua  wao wenyewe na badala yake watumie muda huo kuwasikiliza vijana kupitia mikutano ya hadhara ili kupokea na kutatua kero zinazowakabiri.

"Sitafurahi nikisikia kiongozi umeenda kwenye kikao chako halafu unapiga maneno mwanzo mwisho na watu wanabaki kukusikiliza wewe tu hapo hautaelewa ni nini wanachokitaka ila wewe utataka waelewe ni nini unachokitaka utakuwa unaonekana kiongozi ambaye haujasimama sawasawa ni lazima usikilize watu unaowaongoza hapo ndipo utabaini changamoto zao na utakaposhughulika na changamoto zao na wewe ndipo utahesabika kuwa kiongozi makini kwahiyo kuanzia mwezi ujao kwenye vikao,mikutano na makongamano yenu mtakayofanya waachieni vijana wajadili watoe mawazo nyinyi kazi yenu kusikiliza,kupokea na kutafuta ufafanuzi hicho ndicho nataka kukiona kinafanyika"

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti Benard amewaagiza viongozi hao kuendelea kuwaelimisha vijana na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadae mwaka huu 2024 pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

"Tunalo jambo kubwa la kitaifa kuanzia mwaka huu 2024 katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka kesho 2025 kila Mtanzania haki yake na wajibu wake unaanza kwa kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura, viongozi wangu nendeni mkahakikishe kila Mtanzania amejiandikisha "

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga vijijini Bwana Emmanuel Nganga Golani amewataka vijana kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo wanayoishi ili kujikwamua kiuchumi.

"Mheshimiwa Mwenyekiti zipo fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika maeneo tunayoishi ambazo nilijitahidi sana kuzieleza wakati wa ziara zangu zinazoweza  kuwasaidia vijana wetu kujikwamua kiuchumi mfano kata ya Didia iliyochangamka kiuchumi,Mwakitolyo kata yenye migodi mingi kwahiyo vijana niwaombe tutumie fursa hizo kuinua kipato chetu"

Katibu wa Chama Wilaya ya Shinyanga Vijijini Bi.Erenestina Richard amewasisitiza vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa chama na  serikali  ili kupata nafasi ya kulitumikia taifa kupitia uongozi.

"Vijana changamkieni fursa za kugombea nafasi mbalimbali za chama na uongozi wa serikali muda utafika tutatangaza nafasi za kugombea nendeni mkachukue fomu za kugombea mahali popote,jazeni kisha rudisheni zikiwa zimejazwa vizuri ili mlitumikie taifa katika katika mbalimbali za uongozi"

Sanjali na hayo, Mjumbe wa baraza la UVCCM taifa Monalisa Daniel Faustine amewasisitiza vijana kuendelea  kushirikiana na  viongozi wa serikali ili kuchochea maendeleo ya kila mmoja na taifa kwa ujumla.

"Sisi ni nguzo tunayotegemewa na serikali yetu tuendelee kuwaunga mkono viongozi wetu wakati wote wa majukumu yao tushirikiane,tupendane na tifanye kazi katika umoja ili tuchochee maendeleo ya taifa letu"

Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Beach Corner kata ya Didia ukijumuisha viongozi mbalimbali wa UVCCM  Wilaya ya Shinyanga Vijijini wenye lengo la kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili vijana katika maisha.


Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga vijijini  Emmanuel Nganga Golani akizungumza wakati wa kikao.

 

Post a Comment

0 Comments