Na Mapuli Kitina Misalaba
Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Daniel Kapaya, ameanza ziara yake mkoani Geita, ambapo leo amefika katika Ofisi ya
Polisi Mkoa wa Geita na kupokelewa na ACP Mimata, Mkuu wa Operesheni wa Mkoa wa
Geita, pamoja na SSP Thomas Mtikatika, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Geita, kwa
niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Sofia Jongo.
Uongozi wa jeshi la polisi unathibitisha mchango
mkubwa wa SMAUJATA katika kuibua na kupinga vitendo vya ukatili kwenye jamii, zikiwemo mimba za utotoni, ulawiti, ubakaji, ukeketaji, na ajira za watoto.
ACP Mimata anasema SMAUJATA imekuwa msaada mkubwa
katika kufichua vitendo vya kihalifu na kuimarisha ulinzi wa haki za watoto na
wanawake.
Kwa upande wake, Daniel Kapaya ameliomba jeshi la
polisi kuendelea kushirikiana na mashujaa wa SMAUJATA katika utekelezaji wa
majukumu yao.
Amesisitiza kuwa mashujaa wanahitaji msaada wa usafiri
na kushirikishwa kwenye vikao au kampeni yoyote inayohusiana na kupinga ukatili
ili waweze kutoa elimu kwa jamii kwa ufanisi zaidi.
Kapaya pia amewaelekeza viongozi wa SMAUJATA katika ngazi zote kuanzia vitongoji hadi mkoa kuendelea kufikia maeneo tofauti kwa lengo la kutoa elimu ya kupinga ukatili bila kujali ukabila, dini, ukanda au itikadi za kisiasa.
Amesisitiza kuwa ni muhimu viongozi wasioonyesha
ushirikiano kuchukuliwa hatua za kupunguzwa mamlaka ili kuongeza ufanisi wa
utekelezaji wa majukumu ya SMAUJATA.
Katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Geita, Bw. Frank
Kapiligi, amemshukuru Katibu wa Kanda ya Ziwa kwa kufanya ziara katika Mkoa wa
Geita na kuweza kujenga uwezo mkubwa wa kiutendaji. Kapiligi anasema Geita
imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu wa Kanda ya Ziwa na inaahidi
kuyatekeleza kwa ufanisi.
Ziara hii inaendelea kuboresha ushirikiano kati ya SMAUJATA na jeshi la polisi kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii.








Post a Comment