Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, leo Alhamisi tarehe 19.12.2024, amempa daraja takatifu la Ushemasi Frateri Deusdedith Nkandi wa Jimbo Katoliki Shinyanga, kupitia Misa takatifu ya Ushemasi ambayo imefanyika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga.
Kardinali Pengo amemtaka Shemasi huyo mpya kwenda kuwa mjumbe wa amani bila kuongozwa na hisia za kutaka kulifurahisha kundi fulani la watu, na badala yake atekeleze majukumu aliyopewa kwa kufuata mafundisho ya Kristo.
Amemsihi kamwe kutotafuta visingizio katika kufanya kazi ya Mungu aliyokabidhiwa na badala yake atambue sababu ambayo Mungu amemuitia.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amewashukuru wote waliomwezesha Shemasi Nkandi kufikia daraja hilo, wakiwemo wazazi, walimu, Mapadre waliomlea pamoja na waamini.
Pia amewaalika waamini wa Jimbo la Shinyanga kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya miito ambayo jimbo analijalia, ambayo inazidi kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Askofu Sangu amemtuma Shemasi Nkandi kwenda kufanya kazi katika Parokia ya Mtakatifu John- Bariadi mkoani Simiyu.
Pia ametangaza tarehe ambayo Shemasi Nkandi atapewa Daraja la Upadre kuwa ni Julai 17 mwaka 2025.
Misa ya Ushemasi imehudhuriwa na Mapadre, Mashemasi kutoka nje ya Jimbo la Shinyanga, watawa, Mafrateri wa Jimbo la Shinyanga ambao wako mwaka wa uchungaji mkubwa na viongozi wa Serikali wakiwemo Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi na Katibu wa Mbunge Samweli Jackson ambaye alimwakilisha Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini, Paschal Patrobas Katambi.
Post a Comment