Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwa niaba ya Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amemkabidhi Monsinyori Dominic Makalanga Mgata wa jimbo la Shinyanga, hati maalum ya kupewa hadhi ya Umonsinyori iliyotoka kwa Baba Mtakatifu Fransisko.
Monsinyori Mgata amekabidhiwa hati hiyo kwenye Misa ya utolewaji wa daraja la Ushemasi kwa Frateri Deusdedith Nkandi, iliyofanyika leo katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga.
Naye Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amempongeza Monsinyori Mgata kwa juhudi alizozifanya katika kuchangia ustawi wa Kanisa, hatua ambayo imemfanya Baba Mtakatifu Fransisko kutambua mchango wake katika Jimbo la Shinyanga.
Monsinyori Dominic Makalanga Mgata anayefanya utume wake katika Parokia ya Nyalikungu- Maswa, alitangazwa kupewa hadhi ya Umonsinyori na Baba Mtakatifu Fransisko mnamo Desemba 9, 2024, ambayo ni heshima ya pekee wanayopewa Mapadre wachache kwa mapendekezo ya Maaskofu wao kutokana na mchango mkubwa walioufanya katika ustawi wa Kanisa.
Post a Comment