" TRA YAWASHUKURU WALIPA KODI KWA KUWA NGUZO YA MAENDELEO YA TAIFA

TRA YAWASHUKURU WALIPA KODI KWA KUWA NGUZO YA MAENDELEO YA TAIFA


Na Mwandishi Wetu, Misalaba Media
 
Katika jitihada za kuimarisha uhusiano na wadau wa maendeleo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutambua na kushukuru mchango wa walipa kodi kwa moyo wa dhati. Mkurugenzi wa Sheria wa TRA, Bw. Elisha Shigela, akiwa mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa TRA, alifanya ziara maalum kwa wafanyabiashara maarufu mkoani Shinyanga na kuwapongeza kwa kujitoa kwao katika ulipaji wa kodi kwa hiari na wakati.

Ziara hiyo ilianza katika kampuni ya Gilitu Enterprise Company, ambapo Bw. Shigela alisema:
"Kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, napenda kuwashukuru kwa moyo wenu wa uzalendo mnapoendelea kulipa kodi kwa hiari. Serikali haiwezi kufanikisha malengo yake bila ninyi, walipa kodi. Kila barabara inayojengwa, kila shule inayojengwa, na kila huduma ya afya inayotolewa ni matokeo ya mchango wenu mkubwa. Asanteni kwa kuwa mabalozi wa maendeleo ya taifa letu."

Kwa upande wake, Bw. Gilitu Nila Makula, Mkurugenzi wa Gilitu Enterprise, alieleza safari yao ya kibiashara na namna TRA imewasaidia kufanikisha malengo yao. Alisema:
"Tulianza safari ngumu mwaka 2017, lakini kwa msaada wa TRA na serikali, tumeweza kuimarika sokoni. Najivunia kulipa kodi kwa sababu kodi hizi ndizo zinazoleta miundombinu bora, maji, umeme, na hata ulinzi. Napenda kuipongeza TRA kwa mabadiliko makubwa katika ushirikiano na walipa kodi. Kwa sasa, tunakaa mezani, tunajadili changamoto, na tunapata suluhisho kwa amani. Asanteni sana."

TRA ilimpatia zawadi ya shukrani Bw. Makula kwa mchango wake mkubwa na kutambua umuhimu wa kazi yake katika kuchangia maendeleo ya taifa.

Ziara hiyo ilifuatiwa na kutembelea kampuni ya East Africa Spirit (T) Ltd na Gaki Investment Co. Ltd, ambapo Mkurugenzi wa kampuni hizo, Bw. Gasper Kileo, alipokea salamu za shukrani kutoka kwa Bw. Shigela kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA. Bw. Shigela alisema:
"Unatoa mchango mkubwa kwa taifa, na TRA inatambua kazi yako. Kodi unazolipa ni kiungo muhimu cha maendeleo ya nchi. Tunakutia moyo uendelee na moyo huu wa kizalendo kwa sababu taifa letu linajengwa na wanannchi wenyewe kupitia kodi."

Bw. Kileo aliwashukuru TRA kwa kutambua juhudi zao na kueleza furaha yake kuhusu TRA mpya inayoweka mkazo kwenye ushirikiano na walipa kodi.

Ziara ilihitimishwa kwa kutembelea mfanyabiashara wa bidhaa mbalimbali, Bi Clecensia Ernest, ambaye naye alitoa shukrani kwa TRA kwa kutambua mchango wa walipa kodi. Alisema:
"Kupitia kodi tunapata huduma muhimu kama shule, hospitali, na miundombinu. Nawashukuru TRA kwa kushirikiana nasi na kututia moyo. Ushirikiano huu utatupeleka mbali."

TRA imeahidi kuendelea kushirikiana na walipa kodi kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kwa hiari, huku ikiendelea kutoa huduma bora na kuwapa msaada unaostahili.



















Post a Comment

Previous Post Next Post