" WANANCHI WANA UHURU WA KUTOA MAONI KUPITIA MIKUTANO YA HADHARA

WANANCHI WANA UHURU WA KUTOA MAONI KUPITIA MIKUTANO YA HADHARA

Wananchi wameshauriwa kuitumia mikutano ya hadhara ambayo inaitishwa na wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji kutoa maoni yao, kwa kuwa ndiyo fursa pekee inayowapa uhuru wa kujieleza.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa wenyeviti wa Mitaa,vijiji na vitongoji katika Manispaa ya Shinyanga Nasor Bhoke Warioba, wakati akizungumza kupitia mjadala wa uhuru wa kujieleza katika ngazi ya Serikali za mitaa na vijiji, ambao umeendeshwa na Redio Faraja kwa kushirikiana na Umoja wa Club za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

Warioba amebainisha kuwa, njia pekee ambayo wanaitumia wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji kuwapa nafasi wananchi kutoa maoni yao ni kupitia mikutano ya hadhara ambayo kulingana miongozo ya utendaji wao inapaswa kufanyika kila robo ya mwaka (mara nne kwa mwaka)

Amesema kupitia mikutano hiyo ambayo hubeba Ajenda mbalimbali ikiwemo za ulinzi na usalama pamoja taarifa ya mapato na matumizi, wananchi wanaweza kuhoji au kushauri juu ya jambo lolote ambalo wanaamini litakuwa na mchango katika ustawi wa eneo lao.

Bwana Nasor amewataka wananchi kutambua nafasi waliyonayo katika kuchangia ustawi wa maeneo yao na kwamba, kutoshiriki kwenye mikutano ya hadhara inayoitishwa na viongozi wao ni kujikosesha fursa muhimu ya kutoa maoni hatua ambayo inawafanya baadhi yao kubaki wakitoa lawama kwa viongozi hao.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kitangili Bi. Habiba Jumanne Ramadhani ambaye alishiriki mjadala huo, amesema kwenye mtaa wake amekuwa akiitisha mikutano ya hadhara kila pale inapohitajika ikiwemo ile ya kisheria, na amekuwa akipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi ambao hufika kwa wingi na kujadili pamoja namna ya kushughulikia masuala mbalimbali ya mtaa, ambapo pia Mtendaji wa mtaa huo husoma taarifa ya Mapato na matumizi 

Hata hivyo, miongoni mwa wananchi waliochangia mjadala huo wameeleza kutoridhishwa na utendaji wa baadhi ya viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji, kutokana na hulka yao ya kutaka kutumia madaraka waliyonayo kujinufaisha na kutoitisha mikutano ya hadhara kama inavyotakiwa, hatua ambayo inawafanya wananchi wakose ufumbuzi wa kero na changamoto zinazowakabili, ikiwemo ufafanuzi wa mambo mbalimbali ambayo hawayaelewi.

Wananchi wamewataka viongozi wote wa mitaa,vijiji na vitongoji kutimiza kikamilifu wajibu wao, kufanya kazi kwa njia shirikishi ikiwemo kuitisha mikutano ya hadhara ili kila mwananchi apate fursa ya kuchangia maendeleo ya eneo lake na kufahamu mipango iliyopo.

Post a Comment

Previous Post Next Post