Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amesema dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa foleni na msongamano wa magari Jijini Dodoma unapungua pamoja na kusisimua uchumi wa Mkoa huo kupitia huduma za usafiri na usafirishaji.
Mhe. Ulega amebainisha hayo leo Jumamosi Juni 14, 2025 wakati wa hotuba yake kwenye Mkutano wa hadhara wa Rais Samia, Nala Mkoani Dodoma, mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa Msalato pamoja na barabara ya mzunguko ya nje ya Jiji la Dodoma, akimshukuru kwa maelekezo na msukumu wake katika miradi ya ujenzi nchini.
Aidha Kando ya kupunguza msongamano, Ulega amebainisha kuwa barabara hiyo ya mzunguko wa nje ya Jiji la Dodoma yenye urefu wa Kilomita 112.3 itaongeza pia fursa za kiuchumj kwenye usafiri na usafirishaji, kukuza utalii mkoani humk pamoja na kuimarisha shughuli za kiuchumi ikiwemo shughuli za viwanda na Kilimo.
Amebainisha pia kwamba ni mpango wa serikali kupitia mkopo wa masharti nafuu wa Benki ya dunia, kuweza kupanua barabara ya Chamwino mpaka kwenye mzunguko wa barabara Kimbinyiko na kuwa na njia sita, ikiwemo mbili katikati kwaajili ya mabasi yaendayo haraka.
Aidha serikali ya awamu ya sita pia imepanga kupanha barabara ya Dodoma- Arusha kuanzia kwenye eneo la Njiapanda ya wajenzi hadi Njiapanda ya Msalato yenye urefu wa Kilomita 8.5 ambapo Waziri Ulega amemshukuru Rais Samia kwa kutoa kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi.
Aidha katika kupunguza msongamano Jijini Dodoma, serikali pia inajenga barabara ya kutoka Uwanja wa ndege wa Kimataifa Msalato kupitia Mji wa serikali mpaka Ikulu ya Chamwino ili kurahisisha huduma za usafiri kutoka Ikulu na Mji wa serikali bila kulazimika kupita katikati ya Jiji hilo la Dodoma.
Post a Comment