Na Lydia Ezra Lugakila,Misalaba Media-
MissenyiMbunge wa Jimbo la Missenyi mkoani Kagera, Frolent Kyombo, anatarajia kufanya ziara ya siku nane kwa lengo la kusoma utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata zote 20 kuanzia Juni 16 hadi Juni 19, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mhe, Kyombo amesema kuwa amekuwa akizunguka katika kata mbalimbali na kwamba ziara hii ni muhimu sana.
"Nitakwenda ndani ya kata kusoma utekelezaji wa ilani, na hii ni hatua muhimu" alisema mbunge huyo.
"Zamani tulikuwa tukifanya hivyo ndani ya ukumbi wa wilaya mara moja, lakini sasa tuna wajumbe zaidi ya 6,000 ndani ya kata," alisema.
Kyombo aliongeza kuwa sio rahisi kuwaleta wajumbe wote hao sehemu moja, hivyo ni lazima watu wapite katika kila kata ili kuona kazi zilizofanyika katika maeneo yao.
"Mimi kama mbunge, nikiulizwa, nasema ‘barabara hii hapa, shule hii hapa, darasa hili hapa,’ ili wananchi waweze kuthibitisha kweli kile ambacho kimefanyika katika kata kwa kipindi cha miaka mitano chini ya Rais Samia, chama cha Mapinduzi, mbunge, na diwani," alisema Kiongozi huyo.
Aidha, amesema kuwa wana orodha ya mambo yaliyofanyika ndani ya kata na kiwango cha fedha kilichotumika ili wananchi waweze kuyaona na kutoa nafasi kwa viongozi hao kuongoza vizuri hasa katika kipindi kinachofuata.
Hata hivyo, amewashukuru madiwani wote kwa ushirikiano wao mzuri na kuwataka kuendeleza mshikamano ulioimarika.
Post a Comment