" LIGI YA DUMISHA AMANI KUENDELEA KUTIMUA VUMBI HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA, VIJANA WAASWA KUTUMIA FURSA KUINUA VIPAJI

LIGI YA DUMISHA AMANI KUENDELEA KUTIMUA VUMBI HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA, VIJANA WAASWA KUTUMIA FURSA KUINUA VIPAJI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Ligi ya Dumisha Amani imeanza kwa kishindo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ikihusisha timu 32 kutoka kata 14, huku vijana wakihamasishwa kutumia fursa hiyo kuendeleza vipaji na kudumisha amani nchini.

Uzinduzi rasmi wa ligi hiyo umefanyika Juni 8, 2025 katika Kata ya Tinde, ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi.

Mdhamini mkuu wa ligi hiyo, Fadhili Nafutari ambaye pia ni mdau mkubwa wa michezo, amewapongeza waandaaji wa mashindano hayo kwa lengo la kuhamasisha amani, kuibua vipaji na kusaidia vijana kufikia ndoto zao kupitia soka.

“Nipende kuwaasa kwa mechi hizi zitakazoendelea kuchezwa kwa timu zote 32, najua wote watafanya vizuri. Niwaase ndugu zangu vijana, mcheze mpira kwa kujituma. Mpira ni maendeleo, mpira ni ajira. Mtumie fursa hii vizuri ili mkuze vipaji vyenu muweze kufika mbali,” amesema Nafutari.

Aidha, amesema michezo ni daraja la kuunganisha jamii na kufikisha ujumbe wa kudumisha amani, huku akitoa rai kwa vijana kuitumia Ligi ya Dumisha Amani kama jukwaa la kujitangaza na kupata nafasi ya kusajiliwa na vilabu vikubwa.

Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi ambaye pia ni Polisi Jamii Kata ya Tinde, Beda Lutego, amesema michezo hiyo ni njia mojawapo ya kuimarisha mshikamano miongoni mwa wananchi, na pia inaweza kusaidia katika kuwabaini wahalifu walioko kwenye jamii.

“Tuitumie michezo hii kuendelea kushirikiana kama jamii, kuimarisha amani na kuwafichua wale wachache wanaotaka kuivuruga,” amesema Lutego.

Mratibu wa ligi hiyo, Sungi Leonard amesema mashindano hayo yanahusisha timu kutoka kata 14, na zitacheza hatua ya makundi hadi kufikia fainali ifikapo Julai 6, mwaka huu 2025.

Baadhi ya wachezaji, wameeleza kufurahishwa na kuanzishwa kwa ligi hiyo, wakisema ni fursa adimu kwa vijana kuonyesha uwezo wao mbele ya wadau wa michezo na kupata nafasi ya kutimiza ndoto zao za kucheza soka la kulipwa.

Ligi ya Dumisha Amani inaelezwa kuwa mojawapo ya michuano inayosisimua zaidi mwaka huu mkoani Shinyanga, huku matumaini yakiwa makubwa kwamba itachangia katika kukuza vipaji, kuleta mshikamano na kudumisha amani katika jamii.

 

Mratibu wa Ligi ya Dumisha Amani Sungi Leonard,akizungumza.


 

 

Post a Comment

Previous Post Next Post