Na Lydia Lugakila, Misalaba Media-Bukoba
Walimu wa shule za msingi na sekondari kutoka wilaya ya Missenyi na Bukoba, mkoani Kagera, wameiomba Serikali kuanzisha mitaala ya elimu ya fedha kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu lengo likiwa ni kuwajengea wanafunzi uelewa mzuri juu ya matumizi sahihi ya fedha.
Elimu hiyo imefanyika katika uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba na kuwakutanisha wanachama takribani wote.
Wakizungumza na waandishi wa habari, walimu hao waliopata mafunzo kutoka chama cha ushirika cha akiba na mikopo kinachohudumia watumishi wa umma wa wilaya za Missenyi na Bukoba Burute SACCOS LTD wamesisitiza kuwa ukosefu wa elimu ya matumizi ya fedha ni changamoto kubwa inayowakabili watu wengi, na husababisha matumizi yasiyo na mpangilio mzuri hivyo kuiomba Serikali kuona namna ya kuisaidia katika suala la elimu ya fedha.
Auson Pastory kutoka Wilaya ya Missenyi amesisitiza umuhimu wa elimu ya fedha katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi.
Naye Bi Hilda Manyanga kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ameongeza kuwa ni muhimu vijana wao wawe na uelewa mzuri wa matumizi ya fedha.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Burute SACCOS LTD Charles Tegamaisho, amesema zaidi ya walimu 1,000 wamepatiwa elimu sahihi juu ya matumizi ya fedha, hatua itakayosaidia kuongeza vipato vyao.
Tegamaisho pia alitaja lengo la mafunzo hayo kuwa ni kuwapatia elimu ya fedha na kwamba chama hiki kimekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo haya kila mwaka hivyo suala hilo ni endelevu.
Bi. Enikia Bisanda, Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Kagera, amewashauri walimu kuzingatia umuhimu wa kuweka akiba katika vyama vya ushirika ili kujiepusha na uharibifu wa fedha.
Ameishukuru bodi ya Burute kwa kutoa mafunzo bure, ambayo katika sehemu nyingine yanagharimu hadi shilingi laki tano.
Mrajisi Bisanda aliongeza kuwa chama hicho kimefikia msingi wa tano wa ushirika, ambao ni elimu, mafunzo, na taarifa.
Akitaja faida za elimu ya fedha, amesema inaimarisha nidhamu, inakabili madeni yasiyo ya lazima, inasaidia kutokukopa fedha, na inachochea ukuaji wa mtaji.
Naye Meneja wa Burute Saccos Ltd Godian Stephen kwa niaba ya Mwenyekiti wa Burute, amesema chama kitaendelea kuwapatia mafunzo na elimu wanachama, viongozi, na watendaji ili kuimarisha uelewa wa dhana ya ushirika.
Post a Comment