" WANAOTUPA TAKA OVYO MANISPAA YA BUKOBA WAONYWA.

WANAOTUPA TAKA OVYO MANISPAA YA BUKOBA WAONYWA.


Na Lydia Lugakila, Misalaba Media-Bukoba

Katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, wananchi wa Manispaa ya Bukoba, Mkoani Kagera wametakiwa kuacha tabia ya kutupa taka ovyo, kwani inaweza kusababisha magonjwa ya kuambukiza na kuchafua taswira ya mji.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa kitengo cha usimamizi wa taka na usafi wa mazingira, Tambuko Joseph, wakati akiongea na waadishi wa habari ambapo amesisitiza umuhimu wa usafi wa mazingira na kubainisha kuwa wapo baadhi ya wananchi wanaofanya vizuri lakini wengine wanaendelea na tabia ya kutupa taka barabarani na kwenye mito.

Joseph amefafanua changamoto zinazojitokeza, hasa wakati wa mvua ambapo amesema taka nyingi hutupwa kwenye maeneo yasiyo sahihi.

 "Tumekuwa tukichukua jitihada ya kuziondoa taka hizo kabla hazijaingia ziwa Victoria"alisema Joseph

Ameweka wazi kuwa sheria zipo zinazowabana wale wanaoshindwa kutii kanuni za usafi, akiwemo kuwapeleka mahakamani. 

Joseph ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha  katika masuala ya usafi, akieleza kwamba asilimia 75 ya magonjwa ya kuambukiza yanatokana na uchafu wa mazingira. 

Kwa upande mwingine, Halmashauri ya wilaya ya Bukoba imeadhimisha siku hiyo kwa kupanda miti mia tano ya matunda katika Hospitali ya Wilaya, chini ya usimamizi wa Dr. Kisanga Makigo.

 Dr. Kisanga amehimiza jamii kuendelea kupanda miti ili kulinda mazingira na kujitahidi kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila tarehe 5 Juni, na mwaka huu kauli mbiu ni "Mazingira yetu na Tanzania ijayo tuwajibike sasa dhibiti matumizi ya plastiki"

Post a Comment

Previous Post Next Post