" TUHUMA ZA KUKUTWA NA VIUNGO VYA BINADAMU KAGERA

TUHUMA ZA KUKUTWA NA VIUNGO VYA BINADAMU KAGERA

Na mwandishi wetu
Kagera 

Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera linawashikilia wanaume wawili kutoka mkoani Songwe kwa tuhuma za kukutwa na viungo vya binadamu, tukio linalozua maswali mengi kuhusu usalama na maadili ya kijamii.

Watuhumiwa hao ni Kelvin Piason Mdolon (42), mkazi wa Mnyiha na mganga wa kienyeji pamoja na Randani Seme Mlomo (64), mkazi wa Mnyamwanga ambaye ni mtumishi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Vwawa wilayani Mbozi, mkoa wa Songwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Blassius Chatanda, alithibitisha kuwa Kelvin Mdolon alikamatwa tarehe 17 Juni mwaka huu akiwa na viungo vya binadamu na alidai kuwa alihitaji kuvitumia kwa matumizi yake binafsi.

Katika mahojiano, Kelvin alimtaja Randani Mlomo kama aliyempatia viungo hivyo kutoka chumba cha kuhifadhia maiti. 

Hii ilifanya polisi kumkamata Randani na kuanzisha uchunguzi wa kina ili kubaini undani wa tukio na mtandao wake iwapo upo.

Kamanda Chatanda aliwahimiza wananchi wa Kagera kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za matukio yasiyo ya kawaida. Aidha, alitoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na shughuli za uganga wa jadi bila kuwa na vibali halali, akisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili kudhibiti vitendo vinavyohatarisha maisha ya watu na kukiuka sheria za nchi.

Upelelezi wa tukio hilo unaendelea.

Post a Comment

Previous Post Next Post