Na Lucas Raphael,TaboraTAASISI ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imezindua Kampeni ya uanzishaji na uimarishaji madarasa ya kisomo cha Elimu ya Watu Wazima (EWW) ambayo itaanza kutekelezwa katika halmashauri na Mikoa yote hapa nchini.Hafla ya uzinduzi wa Kampeni hii Kitaifa imefanyika jana katika ukumbi wa shule ya sekondari Magreth Sitta, Wilayani Urambo Mkoani Tabora na kuhudhuriwa na mamia ya wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wanafunzi.Akizindua Kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Paul Chacha, Mkuu wa Wilaya ya Urambo Dk Hamis Mkanachi amepongeza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa kuanzisha kampeni hii ili kuongeza hamasa kwa jamii.Ameeleza kuwa katika karne hii, elimu ya watu wazima si suala la hiari tena bali ni hitaji la msingi katika kujenga taifa lenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.‘Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 17 ya Watanzania watu wazima sawa na watu mil 10.4 hawana stadi 3 za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) na kwa Tabora asilimia 32 ya wakazi wake sawa na watu mil 1.85 hawana stadi hizo’, ameeleza.Dk Mkanachi amebainisha kuwa takwimu hizi zinatoa wito kwa viongozi, watunga sera na jamii kwa ujumla kuchukua hatua za makusudi za kupanga mikakati ya muda mfupi na mrefu ili kuondoa changamoto hii kwa watanzania.‘Afisa Elimu Mkoa hili ondoka nalo, nendeni mkaweke mkakati wa dhati wa kufikia wananchi wote, wahamasisheni kujiunga na madarasa ya kisomo hiki ili kupunguza idadi ya wasiojua Kusoma, Kuhesabu na Kuandika’, ameagiza.Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Profesa Philipo Sanga ameeleza kuwa kampeni hii ni muhimu sana kwa kuwa itasaidia kupanua wigo wa uwepo wa madarasa ya kisomo cha EWW hapa nchini.Amesisitiza kuwa madarasa haya yanatoa fursa kwa wasio na stadi za KKK kujumuishwa katika shughuli mbalimbalio za maendeleo hivyo kujenga jamii imara na yenye ustawi mzuri kiuchumi.Profesa Sanga amebainisha kuwa wanatarajia kuanzisha Vituo vya Mafunzo ya stadi za KKK katika Mikoa yote (Community Learning Centers) hivyo akaomba wadau kuunga mkono kampeni hiyo ili kutimiza kwa vitendo dhana ya elimu bila ukomo.Afisa Elimu Mkoa wa Tabora Upendo Rweyemamu amepongeza TEWW kwa kuanzisha Kampeni hii na kuja na mkakati wa kujengwa vituo vya mafunzo ili kusaidia maelfu ya watanzania waliokosa fursa hiyo ili waweze kujiendeleza. Mwisho. 

Post a Comment