" RC MTANDA AWAASA WANAHABARI KUZINGATIA MAADILI NA SHERIA KATIKA KURIPOTI UCHAGUZI

RC MTANDA AWAASA WANAHABARI KUZINGATIA MAADILI NA SHERIA KATIKA KURIPOTI UCHAGUZI

 

Na Mapuli Misalaba, picha na Kadama Malunde


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia maadili na sheria za taaluma yao wakati wa kuripoti taarifa zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa 2025, ili kuepusha taharuki na machafuko katika jamii.


Mtanda ametoa kauli hiyo leo, Agosti 7, 2025, wakati akifunga semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na Jeshi la Polisi, iliyofanyika jijini Mwanza kwa lengo la kujengeana uwezo kuelekea uchaguzi huo.


Amesema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, kwa kuandika habari sahihi, zenye kuelimisha jamii badala ya kuchochea vurugu au migawanyiko ya kijamii.


 "Uchaguzi ni tukio nyeti, hivyo waandishi wa habari wanapaswa kuwa makini, waandike kwa usahihi na kuzingatia sheria na maadili ili kuepuka kueneza taarifa zenye kuleta taharuki au uchochezi," amesema Mtanda.

Aidha, amewataka wanahabari kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wa kampeni, ambavyo vinaweza kuwafanya kupotosha ukweli au kuonea wagombea. Vilevile amewasisitiza kutochunguza maisha binafsi ya wagombea bila sababu za msingi.


Katika hatua nyingine, Mtanda amelihimiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linawalinda waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, hususan wakati wa kampeni na upigaji kura, ili wasiingiliwe na vitisho kutoka kwa wagombea au wafuasi wao.


Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari, na kwamba tangu aingie madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan amefungua ukurasa mpya kwa kufungulia vyombo vilivyokuwa vimefungiwa pamoja na kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria kandamizi.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Rodney Mbuya, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi na vyombo vya ulinzi, ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.


Katika semina hiyo, zimewasilishwa  mada mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Waandishi wa Habari, Wajibu wa Polisi na Vyombo vya Habari, Maadili na Sheria za Habari, Matumizi ya Akili Bandia, Utangazaji wa Kampeni, Migogoro, Majanga, na Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuelekea uchaguzi.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, akizungumza.


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Rodney Mbuya, akizungumza.

Post a Comment

Previous Post Next Post