Na Lydia Lugakila
Bukoba
Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Jacob Nkwera, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dokta Samia Suluhu Hassan, kutokana na uzalendo aliouonyesha kwa Bibi Catherine Nathanael wa Manispaa ya Bukoba kwa kumjengea nyumba ya kuishi yeye na wajukuu wake sita, ambao ni watoto yatima.
Nkwera alitoa shukrani hizo Agosti 23, 2025, muda mfupi baada ya hotuba ya mgeni rasmi wa hafla hiyo, mkuu wa mkoa wa Kagera, ambaye ameongoza zoezi la kumkabidhi nyumba Bibi huyo.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa ni mengi ambayo Rais Samia amefanya ya kizalendo hasa kwa watu wanyonge, huku akiwataka Watanzania kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili ambariki awe na upendo zaidi na kuwasaidia watu wengi zaidi.
"Rais wetu ana upendo na ukarimu sana, tuzidi kumshukuru kwa moyo wa huruma," alisisitiza Nkwera.
Aidha, amemshukuru mkuu wa mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwassa, kwa moyo wa kuzijali na kuzifuatilia familia za watu wenye uhitaji.
Kupitia hotuba yake, mkuu wa mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwassa, alieleza kuwa kupatikana kwa nyumba hiyo kulikuja baada ya waandishi wa habari Mkoani Kagera kuripoti taarifa kuhusu mafuriko yaliyomkumba Bibi Catherine mnamo Mei 1, 2024, katika maeneo ya Migera, kata ya Nshambya, ambapo kila kitu kilisombwa na maji, huku nyumba yake ikiwa imebomoka. Hali hiyo ilimstua Rais Samia na kuamua kumjengea makazi mapya katika maeneo ya Buhembe, Manispaa ya Bukoba.
Naye mkuu wa wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, kupitia taarifa fupi aliyoisoma mbele ya mgeni rasmi, alieleza kuwa awali hali ya Bibi Catherine ilikuwa mbaya, ambapo Serikali Mkoani humo chini ya mkuu wa mkoa huo walimpatia misaada mbalimbali, ikiwemo chakula, mavazi, magodoro, na vifaa vya shule kwa watoto wa familia hiyo.
Alimshukuru pia hatua aliyoifanya Bi Adelina ya kuwahifadhi wahanga hao wakati wa mafuriko.
Hata hivyo, Bi Catherine pamoja na wajukuu hao, akiwemo Lovenes Matungwa, mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya Sekondari Hamugembe, wamemshukuru Rais Samia kwa kuwaweka katika mazingira mazuri na salama, huku wakiahidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu katika utendaji wake wa kazi uliotukuka.
GUSA LINK HAPA CHINI👇
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment