Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwenyekiti wa Machifu Tanzania ambaye ni Ntemi wa
Himaya ya Jigoku (Masela) iliyopo Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, Chifu Antonia
Sangalali, ametangaza kufanya ziara katika kila mkoa nchini kwa ajili ya
kumuombea kura mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Samia
Suluhu Hassan, kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza Agosti 24, 2025 katika tamasha lake la
utamaduni linalofanyika kila mwaka kwa lengo la kuendeleza mila, desturi na
utamaduni wa kabila la Wasukuma, Chifu Antonia amesema dhamira yake ni kuhimiza
wananchi kote nchini kumpigia kura za ndiyo Mhe. Samia kutokana na mchango wake
mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Amesema katika kipindi cha uongozi wake, Rais Samia
amefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo ikiwemo
uboreshaji wa huduma za afya, ujenzi wa miundombinu, madaraja pamoja na sekta
nyingine muhimu zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Chifu Antonia ameongeza kuwa yeye pamoja na Machifu
wengine nchini wataendelea kumuunga mkono Rais Samia huku wakihamasisha
wananchi kila kona kuhakikisha wanashiriki uchaguzi na kumpigia kura kwa wingi.
“Tutaenda mkoa kwa mkoa kumuombea kura
Mhe. Samia Suluhu Hassan. Ni kiongozi aliyeonyesha dhamira ya kweli ya
kuwaletea maendeleo Watanzania na hivyo anatakiwa kupewa nafasi ya kuendelea na
uongozi,” amesema Chifu Sangalali.
Mbali na siasa, Chifu huyo ametumia jukwaa hilo
kuhimiza wananchi kuendeleza mila na desturi za asili kwa kuwarithisha watoto
wao ili waweze kukua katika misingi ya maadili mema yanayolinda jamii.
Kwa upande wake Mgeni rasmi katika tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt. Vicent Anney, amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa Chifu Antonia katika
maendeleo ya wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.
Anney ameeleza kuwa serikali itaendelea kushirikiana naye
katika kuimarisha maendeleo ya kijamii, ulinzi na usalama pamoja na kuendeleza
historia na urithi wa utamaduni wa eneo hilo.
“Tunampongeza Chifu Antonia kwa mchango wake mkubwa kwa serikali na
wananchi. Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega naye katika jitihada za
maendeleo na kulinda mila na desturi za asili,” amesema Mkuu wa Wilaya.
Baadhi ya wananchi kutoka himaya ya Jigoku ambao wamehudhuria
tamasha hilo wamepongeza hatua ya Chifu Antonia kuendeleza tamasha la kitamaduni kila mwaka,
wakisema linasaidia kuimarisha mshikamano wa kijamii. Wamesema wataendelea
kumuunga mkono kiongozi wao katika jitihada zake za kuendeleza jamii na kuunga
mkono maendeleo ya taifa.
Tamasha hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa
serikali, wakiwemo Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, viongozi
wa kimila, Mwenyekiti wa waganga wa tiba asili wilayani humo pamoja na wadau wa
maendeleo.
Aidha, burudani za ngoma za asili pamoja na wasanii wa
nyimbo za kitamaduni zilitumbuiza hadhira, akiwemo Nhelemi Mbasando na Ng'wana
Kang'wa, ambao wamekabidhiwa tuzo za heshima kama sehemu ya kutambua mchango
wao katika kuenzi na kuendeleza nyimbo za asili miongoni mwa jamii ya Wasukuma.
Mtemi Antonia Sangalali, akizungumza na wananchi wa
himaya yake ya Jigoku (Masela) kwenye tamasha la utamaduni Agosti 24, 2025.
Mtemi Antonia Sangalali, akizungumza na wananchi wa
himaya yake ya Jigoku (Masela) kwenye tamasha la utamaduni Agosti 24, 2025.


Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt. Vicent Anney
akizungumza katika tamasha hilo la utamaduni himaya ya Jigoku 2025, ambapo
amempongeza chifu Antonia Sangalali kwa kuendeleza utamaduni wa eneo hilo.

Mtemi Antonia Sangalali, akiwaongoza viongozi na wananchi wa himaya hiyo kuimba wimbo maalum ambao ameimba yeye kwa ajili ya kumpongeza Rais Samian na uongozi wake.

Mtemi Antonia Sangalali, akiwaongoza viongozi na
wananchi wa himaya hiyo kuimba wimbo maalum ambao ameimba yeye kwa ajili ya
kumpongeza Rais Samian na uongozi wake.



































Post a Comment