" ACT WAZALENDO WAHAIDI MAPINDUZI YA ELIMU YA KIDIGITALI ZANZIBAR

ACT WAZALENDO WAHAIDI MAPINDUZI YA ELIMU YA KIDIGITALI ZANZIBAR



Pangawe – Chama cha ACT Wazalendo kimeibua matumaini mapya kwa vijana wa Zanzibar baada ya Mgombea wake wa Urais kutoa ahadi ya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, ikiwa ni pamoja na mpango kabambe wa kugawa Laptop mpya kwa kila mwanafunzi wa Sekondari.

Katika mkutano uliohudhuriwa na mamia ya wananchi katika viwanja vya Mzee Mgeni, Jimbo la Pangawe, Mgombea huyo alisema wakati umefika kwa Zanzibar kuondokana na mfumo wa elimu wa kizamani usioendana na dunia ya sasa ya kidigitali.

Akieleza dhamira ya ACT Wazalendo, Mgombea alisema utoaji wa Laptop kwa kila mwanafunzi hautakuwa siasa ya kutoa zawadi, bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa Taifa.

“Teknolojia ndiyo msingi wa maendeleo ya dunia ya sasa. Vijana wetu wanapokosa vifaa vya kidigitali, tunawanyima haki ya kujifunza kwa ushindani. ACT Wazalendo tumedhamiria kubadilisha hali hiyo. Kila mwanafunzi atakuwa na Laptop yake mpya ili kujifunza, kutafiti, na kujiandaa kwa uchumi wa kidigitali,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.

Aliongeza kuwa mpango huu utasaidia kupunguza pengo kati ya wanafunzi wa Zanzibar na wenzao wa nchi nyingine, na hivyo kuwapa nafasi ya kushindana katika masoko ya ajira ya kitaifa na kimataifa.

Mbali na Laptop, Mgombea alibainisha kuwa Serikali yake itaanzisha miji maalum ya kielimu na ubunifu ambayo itakuwa kitovu cha teknolojia, sayansi na ubunifu wa vijana.

“Miji hii itakuwa sehemu ya mafunzo ya vitendo, tafiti za kitaaluma, maabara za kisasa na maeneo ya ubunifu. Vijana wetu watapewa nafasi ya kubuni miradi ya kimaendeleo, badala ya kusoma tu vitabuni bila uhalisia wa maisha,” alisema.

Mgombea huyo alitoa changamoto kuwa mfumo wa elimu wa sasa umekuwa mzigo kwa vijana kwa sababu unawapeleka vyuo vikuu visivyo na maslahi kwao wala kwa Taifa.

“Matokeo yake vijana wengi wanasoma, lakini baada ya kuhitimu wanakosa ajira, hawana kasi, na wanabaki na msongo wa mawazo. Mfumo huu unapaswa kubadilishwa. ACT tutaurekebisha kwa kuhakikisha elimu inamwandaa kijana kujiajiri na kujitegemea,” alisisitiza.

Alieleza kuwa mabadiliko hayo yatahusisha mapitio ya mitaala, kuongeza walimu wenye ujuzi wa kidigitali, na kuhakikisha shule zote zinakuwa na miundombinu ya kisasa inayoweza kuendana na mpango wa Laptop.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo walipokea sera hizo kwa shangwe na matumaini makubwa.

Fatma Khamis, mkazi wa Pangawe, alisema: “Hii ni mara ya kwanza tunasikia mgombea akija na mpango wa kweli wa kuwapa vijana vifaa vya kisasa. Laptop kwa kila mwanafunzi ni ndoto ya muda mrefu. Tukipata hii, watoto wetu hawatabaki nyuma.”

Ali Salum, kijana msomi kutoka Jimbo hilo, naye aliongeza: “Tatizo letu ni kusoma sana lakini mwisho hakuna kazi. Kama ACT wakibadilisha mfumo wa elimu na kutuandaa kujiajiri, basi vijana hatutabaki kuwa tegemezi. Hii ni sera ya kutuondoa kwenye giza.”

Bi Asha Omar, mzazi wa wanafunzi wawili wa Sekondari, alisema: “Hii Laptop itakuwa msaada mkubwa. Hata kama watoto wetu hawatapata kazi serikalini, lakini watapata ujuzi wa kujiajiri kupitia teknolojia.”  

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post