Mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa katika ajali ya gari na pikipiki iliyotokea eneo la Isela, Tarafa ya Samuye, Halmashauri ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, Septemba 25, 2025, majira ya saa 7:00 usiku.
Taarifa hiyo imetolewa na kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi, amesema ajali hiyo ilisababisha kifo cha Sudi Dotto (20) na majeruhi aliyefahamika kwa jina la Noel Paul (18), wote wakazi wa Isela, Halmashauri ya Shinyanga.
Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga inaeleza kuwa ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Kluger lenye namba za usajili ambazo hazikutajwa, ambalo lilikuwa likitokea Tabora kuelekea Mwanza. Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Fabian Manoga (36), ambaye aliligonga pikipiki aina ya SUNLG iliyokuwa ikiendeshwa na marehemu Sudi Dotto.
Majeruhi Noel Paul anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, huku mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari ambaye aliendesha kwa mwendo kasi na bila kufuata sheria za usalama barabarani. Aidha, dereva huyo alihama njia na kuingia upande wa pili wa barabara, jambo lililosababisha kumgonga mwendesha pikipiki aliyekuwa akitokea mbele yake.
Jeshi la Polisi limewataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na majeruhi. Pia, limewataka madereva kuwa waangalifu kila wakati wanapotumia vyombo vya moto.


🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment