
Abiria wa masafa marefu wamepewa elimu ya kutokukaa
kimya pindi wanapoona vitendo vya kuzidisha abiria vikifanywa na makondakta
kwenye magari ya usafiri wakati wa safari.
Akitoa elimu hiyo, Askari Polisi wa Kikosi cha Usalama
Barabarani Mkoa wa Shinyanga, Sajenti David Ndimila, amewataka abiria kuwa
mstari wa mbele katika kukemea na kuripoti vitendo hivyo ambavyo vimekuwa
vikitokea mara kwa mara kwenye safari za masafa marefu.
“Abiria msikae kimya mnapoona makondakta
wanazidisha abiria. Pazeni sauti zenu, mkemee vitendo hivyo kwa kuwa mkiendelea
kunyamaza, mnashiriki moja kwa moja kuvunja sheria na kuhatarisha maisha yenu,” amesema
Sajenti Ndimila.
Aidha, Sajenti Ndimila amesisitiza
kuwa ushirikiano wa pamoja kati ya wananchi na vyombo vya usalama
ndio njia pekee ya kudhibiti uvunjifu wa sheria za usalama barabarani, badala
ya kuwaachia askari pekee jukumu hilo.
“Polisi peke yao hawawezi kufanikisha
jambo hili bila ushirikiano wenu. Ni wajibu wenu kuhakikisha mnakuwa sehemu ya
mapambano dhidi ya vitendo vya uvunjifu wa sheria barabarani,” ameongeza.
Elimu hiyo inalenga kupunguza ajali na madhara
yanayotokana na tabia ya kuzidisha abiria, ambayo imekuwa chanzo cha migongano
na ajali katika usafiri wa masafa marefu.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment