Madereva wa magari ya abiria wamepatiwa elimu ya
usalama barabarani, hususani ulazima wa kusimama kwenye vivuko vya reli ili
kujikinga na ajali zisizo za lazima na kulinda maisha ya abiria
wanaowasafirisha.
Elimu hiyo imetolewa na Askari Polisi wa Kikosi cha
Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga, Sajenti David Ndimila, wakati
akizungumza na madereva hao ambapo amewataka kuacha mazoea ya kupita kwenye
vivuko vya reli pasipo kuchukua tahadhari.
Amesema kuwa ni muhimu kwa madereva kusimama na
kujihakikishia usalama kabla ya kuvuka reli ili kuepusha ajali zinazoweza
kutokea ikiwemo kugongwa na gari moshi.
“Kabla ya kuvuka reli, dereva anatakiwa
kusimama, kuhakikisha hakuna gari moshi linalokuja, kisha kuendelea na safari.
Tabia ya kupuuza sheria hii imekuwa chanzo cha ajali nyingi ambazo zingeweza
kuepukika,” amesema Sgt Ndimila.
Aidha, amewaasa madereva wa magari ya abiria
kuwa mfano bora wa kuigwa na madereva wengine kwa kufuata
sheria za usalama barabarani, ili kuhakikisha abiria wanaosafirishwa wanawasili
salama kwenye safari zao na pia kuepuka majanga yanayoweza kuhusisha treni.
Sajenti Ndimila amesisitiza kuwa elimu ya usalama
barabarani ni jukumu la kila dereva, na kufuata masharti ya usalama kwenye
vivuko vya reli ni hatua muhimu ya kupunguza ajali na kulinda maisha ya
wananchi.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment