Mgombea
Urais kupitia Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Juma Mluya,
akizungumza na waandishi wa habari wilayani Kahama leo septemba 26 baada
ya kuahirishwa kwa mikutano ya kampeni iliyokuwa imepangwa kufanyika
wilayani Kahama na katika manispaa ya Shinyanga kwa nyakati tofauti,
kutokana na kuzorota kwa hali yake ya kiafya.
Na Neema Nkumbi, Kahama
Mikutano
ya kampeni ya Mgombea Urais kupitia Chama cha Democratic Party (DP),
Abdul Juma Mluya, iliyopangwa kufanyika mkoani Shinyanga, kwa nyakati
tofauti, imeahirishwa ghafla kutokana na hali mbaya ya kiafya ya mgombea
huyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo baada ya kuahirishwa kwa mkutano wa kampeni uliokuwa
ufanyika katika kata ya Mhongolo manispaa ya Kahama, Mluya amesema
kuzorota kwa afya yake kumesababishwa na sintofahamu ya kauli ya Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar, Peter Agaton Magwira.
"Makamu
mwenyekiti wa chama chetu kwa upande wa Zanzibar, jana ametoa kauli
kwamba eti, chama kimekaa na kukubaliana kumuunga mkono mgombea urais
Zanzibar kupitia Chama cha Mapindizi (CCM). Amesema Mluya na kuongeza
kuwa
"Kauli
hiyo ni ya kwake, na sio ya chama chetu. Mimi kama mgombea na
mwenyekiti wa chama, kauli hiyo imeniathiri sana kiafya, imeniletea
mshtuko wa moyo na nimeshindwa kuendelea na mikutano ya kampeni
iliyokuwa imeandaliwa ukiwemo huu wa Kahama na kesho Shinyanga."
Amesisitiza
kuwa hakuna kikao rasmi cha chama kilichokaa na kutoa msimamo huo,
hivyo kauli ya Magwira si msimamo wa DP bali ni maoni binafsi, huku
akirejea Katiba ya chama hicho ibara ya 13(2), inayoeleza kuwa
mwenyekiti ndiye msemaji na mlinzi wa katiba ya chama, hivyo taarifa ya
makamu mwenyekiti inapaswa kupuuzwa.
Aidha
amemuagiza Katibu Mkuu wa DP kuandaa barua ya kumsimamisha kwenye
nafasi yake Peter Agaton Magwira, baadhi ya wanachama na wajumbe saba wa
sekretarieti waliokuwa sehemu ya mkutano huo.
wajumbe hao ni Leonard Mkoga, Makame Omary Makame, Mariam Maseka, Juma Kidawa, Salma Mateo, Mkude John Mkude na Zainabu Khamis.
Barua
hizo zitatumika kupeleka mashauri yao katika Kamati ya Maadili, kisha
kufikishwa kwenye Mkutano Mkuu ili wajitete na kuamuliwa adhabu stahiki,
kuanzia onyo, kusimamishwa, au hata kufutwa uanachama.
Hata
hivyo, licha ya kadhia hiyo, Mluya amewahakikishia Watanzania kuwa
ataendelea kusimama kama mtetezi wa walala hoi, huku akisisitiza chama
chake hakitapoteza mwelekeo wa awali wa kampeni.
Ratiba mpya ya mikutano ya Kahama na Shinyanga inatarajiwa kupangwa na kamati husika baada ya tathmini ya afya yake.
Ametoa wito kwa watanzania kudumisha
amani, upendo na mshikamano katika kipindi hiki cha kampeni za kuelekea
uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, huku akiwasihi wanasiasa
kufanya kampeni za kistaarabu na kushindana kwa hoja.
“Hakuna
chama chenye haki miliki ya Tanzania, Kama ingekuwa hivyo, basi
kusingekuwa na sababu ya kuendesha uchaguzi, kwa hiyo tunadi sera zetu,
tushindane kwa hoja.”
Post a Comment