
Na Osama Mohamedi chobo Songea- Misalaba Media, Ruvuma Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeanza rasmi utekelezaji wa mpango wa kufufua kilimo cha kahawa kwa kuwekeza kwenye uzalishaji wa miche bora ya kisasa na kuwaunganisha wakulima kwenye vyama vya ushirika. Afisa Ushirika wa Manispaa hiyo, Given Malik, amesema kuwa wanashirikiana na taasisi mbalimbali kama Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) ili kutatua changamoto zinazowakabili wakulima, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo, elimu ya kilimo bora na masoko ya uhakika.Mkakati huo umepokelewa kwa matumaini makubwa na wakulima, hasa katika kata ya Ndilimalitembo ambako baadhi ya vikundi vya wakulima tayari wameanza kuzalisha miche ya kahawa. Hata hivyo, wakulima bado wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa mbegu, vifaa kama mashine za kupulizia dawa, mikasi ya kisasa, na uhitaji mkubwa wa ruzuku ili kuongeza uzalishaji wa miche. Wakulima wameiomba Serikali kupitia TACRI na TCB kuwapatia ruzuku kama ilivyo kwa mazao mengine ili waweze kuongeza uzalishaji wa kahawa kwa tija.Aidha, Malik amesema Serikali ya awamu ya sita imeweka msukumo mkubwa kwenye kuimarisha ushirika ili kuwawezesha wakulima kupata mikopo ya pembejeo, huduma za ugani na elimu ya ushirika. Kupitia juhudi hizo, Manispaa inalenga si tu kuongeza mapato yake bali pia kuwainua wakulima kiuchumi na kuhakikisha zao la kahawa linakuwa na mchango chanya kwa maendeleo ya jamii nzima ya Songea.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment