Na Lucas Raphael, Misalaba Media -Tabora WAKAZI wa Jimbo la Kaliua Mkoani Tabora na majimbo mengine nchini wametakiwa kuchagua wabunge na madiwani wachapa kazi ambao watawasemea na kusimamia haki zao ipasavyo. Hayo yamebainishwa jana na mgombea ubunge wa Jimbo la Kaliua Mkoani hapa, Magdalena Sakaya kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika vijiji vya Igagala Namba 7 na Namba 5.Amesema kuwa uchaguzi mkuu ni fursa muhimu sana kwa wananchi kupata Viongozi wao kuanzia Rais, wabunge na madiwani, hivyo akawataka kuchagua kiongozi mwenye maono, uwezo na mchapa kazi, vinginevyo watajuta.Kiongozi makini ni yule anayetanguliza mbele maslahi ya wananchi wake, siyo maslahi binafsi, hivyo akawataka kutofanya makosa Oktoba 29, bali wamchague kuwa mbunge wao ili akatetee maslahi yao bungeni.Sakaya amesisitiza kuwa kama watampa ridhaa ya kuwa mbunge atahakikisha huduma za afya zinapatikana kwa katika maeneo yote na vijiji ambavyo havina zahanati atalisimamia ili zijengwe na kuwaondolea kero hiyo.Aidha ameahidi kuwa atahakikisha kata zote ambazo hazina vituo vya afya vinajengwa ili kuwaondolea kero akinamama wajawazito, watoto na wazee ya kutembelea umbali mrefu kufuata huduma hizo katika kata nyingine.Pia ameahidi kusimamia ipasavyo suala la umeme na kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi katika vijiji vyote vya Jimbo hilo, na nguzo za umeme zitafikishwa katika maeneo yote.Kuhusu sauala la mikopo ya asilimia 10 amesema kuwa atahakikisha makundi yote yananufaika na mikopo hiyo na wote wanaostahili kuingizwa katika mfuko wa kunusuru kaya maskini (TASAF) wanaingizwa bila upendeleo.Sakaya amefafanua kuwa serikali imeleta fedha nyingi sana katika Jimbo hilo kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini fedha hizo hazionekani, shida ni nini, kama kuna wanaozitafuna wakamatwe na kuchukuliwa hatua.Amedokeza kuwa hatma ya maendeleo ya wakazi wa Jimbo hilo ipo mikononi mwa kiongozi atakayechaguliwa hivyo akawataka kutofanya makosa bali wachague mtu makini atakayetetea haki zao na maendeleo yao.Mwisho

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment