" BILIONEA AIDAN KUIFUFUA SUNSHINE, KIWANDA KIKUBWA CHA KUCHENJUA DHAHABU CHUNYA

BILIONEA AIDAN KUIFUFUA SUNSHINE, KIWANDA KIKUBWA CHA KUCHENJUA DHAHABU CHUNYA

Kitakuwa na uwezo wa kuchenjua tani 500 kwa Saa 24Kuzalisha Ajira 350 kwa WatanzaniaUkarabati kuchukua  Miezi Miwili ChunyaSeptemba 2024, jina la Bilionea Aidan Andrea Msigwa lilitikisa Sekta ya Madini kama radi katikati ya jua kali kwa kuuza kilo 111.82 za dhahabu. Alivuna zaidi ya shilingi bilioni 20.11 kwa mkupuo mmoja hatua iliyotikisa si tu wadau wa madini, bali iliwaamsha Watanzania wengi hadi kuvuka mipaka ya nchi. Aidan hakutajwa tu kama gwiji wa madini, bali aliwekwa rasmi kwenye meza ya mabadiliko ya kiuchumi ndani na nje ya Tanzania.Baada ya kuvuna mabilioni kutokana na kuuza dhahabu hiyo Aidan hakukimbilia anasa bali alichagua kuwekeza kwa watu baada ya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuinunua Kampuni ya SUNSHINE Group iliyoko Matundasi Chunya iliyokuwa ikimilikiwa na wawekezaji kutoka China. Kwa sasa yupo mbioni kwa kushirikiana na wawekezaji wengine wa China kukifufua kiwanda hicho kikubwa cha kuchenjua dhahabu kilichokuwa kimesimamisha shughuli zake kwa takribani miaka miwili. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuchukua miezi miwili ya ukarabati baada ya taratibu za kiuwekezaji kukamilika. Aidha, kinatarajia kuchenjua tani 500 kwa saa 24, kuzalisha zaidi ya ajira 350 kwa watanzania huku kwa wageni zimetengwa nafasi 40 tu ambapo chini ya ubia huo, wanatarajia kuleta teknolojia.Anasema mbali ya kuinunua SUNSHINE fedha nyingine aliwekeza kwenye ununuzi wa vifaa kwa ajili ya kuendeleza shughuli zake za uchimbaji na uchakataji madini kama ununuzi wa escavetor, magari na mitambo mingine ya kurahisisha kazi zake. Pia, Aidan ni mmiliki wa leseni kadhaa za uchimbaji mdogo wa madini na anazo leseni nyingine ambazo zina uzalishaji  lakini bado hajaanza kuchimba na anaweza kushirikiana na mwekezaji. Vilevile,  anao mtambo wa kuchakata dhahabu  wenye uwezo wa kuchakata tani Mia Mbili 200 kwa saa 24.Hadithi ya Aidan si ya mtu mmoja kutengeneza mabilioni, bali ni simulizi ya kizalendo ya mtu kurejesha matumaini kwa mamia ya familia, vijana, na jamii zinazotegemea Sekta ya Madini kama chanzo cha maisha. Katika mahojiano maalum na timu ya Madini Diary,  amefunguka  juu ya safari yake, maono yake, na kwa nini anasema huu ni mwamko mpya wa kiuchumi na unaong’aa kama jua la asubuhi kwa Chunya na Tanzania .Aidan anasema hakuwahi kufika sekondari. Elimu yake rasmi iliishia darasa la saba, lakini ndoto zake hazikuishia darasani. Tangu mwaka 1989, alihangaika kwenye machimbo, makarasha, kuchenjua, akijifunza kwa vitendo, akikosea na kujirekebisha, akipigania maisha kwa jasho la kweli la mchimbaji mdogo.Lakini leo, licha ya kuvuna bilioni 20.11 za mkupuo na kipato kingine kutoka vyanzo vingine vya uchimbaji, anasema jambo moja analojutia ni kutokuendelea na shule. “Sasa hivi nikikutana na wageni kama hawa mnaowaona, nasemewa na wengine… hilo huwa linaniumiza sana kwasababu ningeweza kuzungumza mwenyewe. Hiki ni kitu ninachojutia kweli japo nilitamani kufanikiwa kwa haraka,” anasema kwa utani wenye uzito. Ndiyo maana licha ya mafanikio yake, anasisitiza kwa nguvu: “Usiache shule kwa tamaa ya mafanikio ya haraka. Mafanikio yatakuja, lakini elimu ni msingi wa kudumu’’, anasema Aidan.Licha ya kuvuna bilioni 20.11 kwa mkupuo mmoja, Aidan Msigwa hakubadilika. Anasema wazi, “Mimi tarehe zote huzimalizia porini si mtu wa starehe, kuanzia tarehe 1 hadi 30, niko porini,’’.Badala ya kupumzika, aliona mafanikio hayo kama hatua ya kwanza ya kuongeza bidii zaidi. Yalimwinua yakamweka mbele ya jamii kama mfano wa kweli, mtu wa kawaida aliyefanikisha ndoto kubwa kwa uvumilivu, uaminifu, na juhudi za kweli. Wengi sasa wanamchukulia kama kioo, wakiona ndani yake picha ya matumaini yao. Amewapa nguvu ya kupambana zaidi, na kwa kiasi kikubwa, amechochea wimbi jipya la uchimbaji na uwekezaji Chunya si kwa wachimbaji wadogo pekee, bali hata wawekezaji wa ndani na nje wanaotaka kuwa sehemu ya hadithi yake. Kwa Aidan alama aliyoiweka haitoshi anataka kwenda mbele zaidi na anasema wachimbaji wadogo wataleta mabadiliko Tanzania.Ombi kwa tasisi za fedha na SerikaliKutokana na mazingira ya shughuli za madini Aidan anatoa ombi kwa taasisi za fedha kuwaamini wachimbaji na wasipewe masharti sawa na wawekezaji wengine kutokana na uhalisia wa shughuli za madini. Pia, anatoa ombi kwa Serikali kutokuhesabu madeni ya nyuma  baada ya kuanzishwa utaratibu mpya wa kutozwa asilimia 2 za Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) katika yote Msigwa hakuacha kuishukuru Serikali kwa kuwezesha mazingira yaliyomfikisha alipo.Na hii kwa ufupi ndiyo SIMULIZI ya Aidan Andrea Msigwa  mmiliki wa Kampuni ya Mdimi Investment, kutoka darasa la Saba hadi Bilioni 20.11: Safari ya uaminifu, uvumilivu na sasa SUNSHINE.  Simulizi zaidi ya Aidan ifuatilie hivi karibuni kupitia Madini Diary.Vision 2030: Madini ni Maisha na UtajiriBilionea Aidan Andrea Msigwa, akizungumza.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post