" HAZINA IPO SHWARI,UWEKEZAJI UNAZIMA POROJO ZA UCHUMI HASI

HAZINA IPO SHWARI,UWEKEZAJI UNAZIMA POROJO ZA UCHUMI HASI

Takwimu mpya za uwekezaji kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) zinathibitisha wazi kwamba uchumi wa Tanzania upo katika hali nzuri na thabiti, zikikanusha vikali madai ya kihuni yanayosambazwa mtandaoni kwamba Benki Kuu imechapisha na kuingiza fedha nyingi kupita kiasi kwenye mfumo. 

Ukweli wa hali halisi ya kiuchumi nchini Tanzania unajionyesha si kwa maneno bali kwa matendo ya wawekezaji, ambao akili zao za kiuchumi hazidanganywi.

Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025/2026, miradi mipya 201 yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 2.54 imesajiliwa na TISEZA. Miradi hii inatarajiwa kuzalisha takriban ajira 20,800 kwa Watanzania. 

Ongezeko hili la ghafla na kubwa la uwekezaji si bahati nasibu; ni matokeo ya moja kwa moja ya sera za kiuchumi zenye mwelekeo wa muda mrefu na mazingira rafiki ya biashara yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Huu ndio uthibitisho mkuu wa kimantiki kwamba wawekezaji wanaamini utulivu na ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Ni kinyume na mantiki kuwekeza mabilioni katika nchi ambayo uchumi wake unayumba kwa sababu ya "fedha nyingi zilizochapishwa."

Hoja kwamba kuna fedha nyingi zimechapishwa na kusambazwa kupita kiasi ingethibitishwa na mfumuko mkubwa wa bei. Kijadi, fedha za ziada zinazokimbiza bidhaa chache husababisha kupanda kwa bei kwa kasi kubwa. Hata hivyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuwa ikisimamia kwa makini sera za fedha, na viwango vya mfumuko wa bei vimeendelea kudhibitiwa, vikibakia ndani ya malengo yaliyowekwa. 

Utulivu huu wa bei unakanusha moja kwa moja madai yoyote ya uwepo wa mzunguko wa fedha usio wa kawaida au uchapishaji wa noti unaohatarisha uchumi. Wawekezaji hawa wanaoleta dola za Marekani Bilioni 2.54 hawawezi kuhatarisha mitaji yao katika uchumi uliojaa mfumuko wa bei usiodhibitiwa.

Mafanikio haya ya uwekezaji yamegusa sekta mbalimbali. Sekta ya Uzalishaji bidhaa viwandani ndio inaongoza kwa ukuaji wa asilimia 42, ikifuatiwa na Makazi/nyumba za biashara (15%) na usafirishaji (14%). Hili linaonesha mabadiliko ya kimfumo kuelekea uchumi wa viwanda. 

Zaidi ya hayo, TISEZA imebainisha kuwa ushiriki wa wawekezaji wa ndani umeongezeka kutoka asilimia 27 hadi 35, jambo linaloashiria ukuaji jumuishi unaohakikisha Watanzania wanachukua nafasi yao katika umiliki wa rasilimali na uzalishaji. Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs) kama Bagamoyo, Kwala, na Buzwagi yamekuwa nguzo kuu za kuvutia mitaji hii.

Kutokana na takwimu zilizopo (na takwimu huwa hazidanganyi) uchumi wa Tanzania unaendeshwa na msukumo thabiti wa kiutendaji na sio porojo za mitandaoni. Takwimu za TISEZA za Dola za Marekani Bilioni 2.54 ni ishara tosha kwamba viongozi na wawekezaji wanatekeleza mikakati yenye tija. 

Katika kipindi ambapo nchi nyingi zinapambana kuvutia mitaji, Tanzania inavuna matunda ya uongozi ulioimarisha miundombinu na kurahisisha mazingira ya uwekezaji, na kuufanya mfumo kuwa rahisi, wa wazi, na wenye tija kwa maendeleo ya nchi nzima. Uwekezaji ndio kielelezo cha kweli cha afya ya uchumi, na kwa sasa, afya ya Tanzania ni njema.


Post a Comment

Previous Post Next Post