" JESHI LA POLISI SHINYANGA LAHIMIZA AMANI NA USHIRIKI WA WANANCHI KATIKA UCHAGUZI MKUU 2025

JESHI LA POLISI SHINYANGA LAHIMIZA AMANI NA USHIRIKI WA WANANCHI KATIKA UCHAGUZI MKUU 2025

Na. Elias Gamaya -Shinyanga

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limewahakikishia wananchi kuwa kutakuwepo amani na utulivu wa kutosha siku ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, na kuwataka wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, ametoa kauli hiyo leo Oktoba 18, 2025, wakati akizungumza na madereva wa bajaji, bodaboda na magari madogo (Hiace) katika eneo la Soko Kuu mjini Shinyanga.

Amesema Jeshi hilo limejipanga kikamilifu kuhakikisha ulinzi na usalama siku ya uchaguzi, na kuwataka wananchi wasiwe na hofu bali wajitokeze kwa amani kwenda kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga tumejipanga vyema kuhakikisha amani inaendelea kutawala siku zote, ikiwemo siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29. Tunawaomba wananchi wote wajitokeze kupiga kura kwa amani, kwani hakutakuwepo vurugu zozote,” amesema Kamanda Magomi.

Aidha, amewaonya watu au makundi yoyote yatakayojaribu kufanya vurugu siku ya uchaguzi, kuacha mara moja nia hiyo, kwani Jeshi la Polisi limejipanga kudhibiti uvunjifu wa amani na halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Bodaboda Manispaa ya Shinyanga, Juma Mrabu, amesema vijana wa bodaboda hawako tayari kutumiwa kuvuruga amani ya nchi siku ya uchaguzi, bali watajitokeza kupiga kura na kurejea kuendelea na shughuli zao za kujitafutia kipato kama kawaida.



 


Post a Comment

Previous Post Next Post