" SADC YAIPONGEZA TANZANIA KWA MAANDALIZI YA UCHAGUZI, YATOA WITO KWA AMANI OKTOBA 29

SADC YAIPONGEZA TANZANIA KWA MAANDALIZI YA UCHAGUZI, YATOA WITO KWA AMANI OKTOBA 29

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imetoa sifa kubwa kwa Tanzania kufuatia maandalizi yake thabiti kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. SADC imesisitiza kuwa mafanikio hayo ni kielelezo cha dhamira ya nchi katika kukuza demokrasia na amani.

Wito huo wa pongezi na amani ulitolewa jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kikosi cha Uangalizi wa Uchaguzi cha SADC (SEOM), uliofanyika Oktoba 21, 2025.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC, Mhe. Richard Msowoya (akizungumza kwa niaba ya Rais wa Malawi, Profesa Arthur Peter Mutharika), alisisitiza umuhimu wa uchaguzi huru, wa haki na unaozingatia misingi ya amani.

"Tunahimiza wapiga kura wote waliojiandikisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani. Huo ndiyo msingi wa kuimarisha demokrasia," alisema Mhe. Msowoya, akitoa wito kwa wadau wote – vyama, asasi za kiraia na vyombo vya habari – kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu.

Ujumbe wa SADC ulishukuru Serikali ya Tanzania kwa ukarimu na kusisitiza kuwa jumuiya hiyo iko tayari kuunga mkono mchakato mzima kwa mujibu wa sheria zake. SADC pia ilieleza kuwa Tanzania ni nchi ya tatu katika ukanda huo kufanya uchaguzi kwa amani na uwazi ndani ya mwezi mmoja.

"Tunawahimiza Watanzania kulinda amani, kuheshimu sheria na kuepuka vurugu. Uchaguzi wa amani ni fahari ya Taifa na urithi kwa vizazi vijavyo," ulisisitiza ujumbe huo.

Kikosi cha SEOM kinaundwa na waangalizi 80 kutoka nchi 10 wanachama wa SADC, ambao watasambazwa katika mikoa yote 27 ya Tanzania Bara na Visiwani kufuatilia hatua zote za uchaguzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post