" WAKUU WA VYOMBO VYA HABARI, WAHARIRI WAANDAMIZI WAKEMEA 'UWENDAWAZIMU WA KIHALAIKI' WATAKA UCHAGUZI WA AMANI

WAKUU WA VYOMBO VYA HABARI, WAHARIRI WAANDAMIZI WAKEMEA 'UWENDAWAZIMU WA KIHALAIKI' WATAKA UCHAGUZI WA AMANI




Na Mwandishi Wetu


Wakuu wa Vyombo vya Habari na Wahariri Waandamizi  wa Tanzania wametoa Azimio la pamoja lenye nguvu wakisisitiza umuhimu wa kulinda amani na kukemea vikali kauli za uchochezi zilizosikika hivi karibuni nchini.


Aidha Wakuu hao wa Vyombo vya Habari na Wahariri Waandamizi walitangaza kuungana na viongozi wa dini na makundi mengine katika kusisitiza umuhimu wa kutunza amani kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba.


Azimio hilo, lililotolewa leo, Oktoba 25 linatoa tahadhari kubwa kuhusu athari za “Uwendawazimu wa Kihalaiki” unaoweza kulisambaratisha Taifa.
Katika Azimio hilo, viongozi hao wa vyombo vya habari wamewataka Watanzania kukataa kuhudhuria karamu ya uchochezi wenye lengo la kuwashawishi kulewa "Uwendawazimu wa Kihalaiki".
Aidha walieleza kuwa mataifa mengi yaliyotumbukia katika machafuko, ikiwemo Rwanda, Kongo, Sudan, na majirani wengine, yamebaki na makovu ya kihistoria kutokana na aina hiyo ya machafuko.


Wamesisitiza kuwa machafuko, mateso na mauaji ya raia yaliyotokea katika nchi hizo yalichangiwa na ubinafsi wa vikundi vya wanasiasa walioamua kutumia propaganda za kugawanya watu bila kujali maslahi mapana ya mataifa yao.


Azimio hilo lilikemea moja kwa moja kauli za hivi karibuni nchini Tanzania, ambazo zimeelezwa kuwa zinazochochea chuki na shari na haziakisi kabisa utamaduni wa Mtanzania. Viongozi hao wa vyombo vya habari walionya kuwa kauli zinazohamasisha wananchi kufanya vurugu, kuchoma vituo vya mafuta, vituo vya polisi na mali nyingine, siyo tu ni kosa kisheria, bali ni kauli zisizoakisi Utanzania na zinazopaswa kukemewa na kila Mtanzania.


Mataifa yanayoingia katika machafuko huanza na kauli chochezi za mtu mmoja mmoja, kisha vikundi, na hatimaye hutengeneza "Uwendawazimu wa Kihalaiki" kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.


Azimio linakumbusha kwamba Tanzania ilipata uhuru kupitia jitihada za majadiliano na hoja, ambapo wanasiasa walipingana bila kupigana. Kutokana na misingi hii, nchi imebaki kuwa kisiwa cha amani na makazi ya matumaini kwa wakimbizi wanaokimbia vita katika nchi zao.

Post a Comment

Previous Post Next Post