Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth GwajimaNa John Bukuku – Dar es Salaam
Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kuwezesha wanawake, vijana na makundi maalum, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kulinda haki za binadamu na kuimarisha ustawi wa jamii nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth Gwajima, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika, katika Kituo cha Ukombozi wa Kusini mwa Afrika jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali imeendelea kutekeleza kampeni mbalimbali za kijamii zinazolenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kukabiliana, kupinga na kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii, huku ikisisitiza mshikamano wa jamii kama nyenzo muhimu ya mafanikio ya mapambano hayo.
Dkt. Gwajima amebainisha kuwa Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Mashujaa wa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, SmaUjataa Sauti ya Watoto Tanzania, CHAWATA, Malezi Bora Network pamoja na vikundi vya watu wenye ulemavu, imefanikiwa kuibua na kuimarisha vikundi vya kizalendo vinavyounga mkono juhudi za Serikali katika kufikia malengo ya ustawi wa jamii.
Amesema vikundi hivyo viliibuka kufuatia kuanzishwa kwa Wizara hiyo na vimeendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali katika kuibua, kukemea na kutoa elimu kwa jamii kuhusu vitendo vya ukatili, ambapo mafanikio yaliyopatikana yametokana na ushirikiano huo wa karibu.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, tangu kuanzishwa kwa kampeni hizo, jumla ya matukio 799 ya ukatili yameripotiwa na kushughulikiwa, huku Wizara ikiendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta mbalimbali, wakiwemo askari polisi 4,542, wasimamizi wa mashauri ya watoto wa kujitolea 15,255, wahudumu wa afya 10,534, maafisa ustawi wa jamii 1,342 pamoja na walimu wa unasihi na malezi 13,755.
Akizungumzia ushiriki wa wanawake katika uongozi, Dkt. Gwajima amesema kuwa kupitia Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2003, Serikali inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha wanawake wanaongezeka katika nafasi za uongozi na maamuzi katika nyanja zote, ikiwemo kwa kushirikiana na vyama vya siasa.
Ameeleza kuwa Serikali inahimiza vyama vya siasa kuandaa sera za ndani zitakazohakikisha nafasi za uongozi zinakuwa wazi kwa wanawake, kuwepo kwa taratibu za uteuzi zisizo na ubaguzi, pamoja na kanuni za maadili ya kisiasa zitakazowalinda wanawake dhidi ya kauli au vitendo vya udhalilishaji.
Hatua hizo, amesema, zimechangia kuongezeka kwa idadi ya wabunge wanawake kutoka asilimia 37.5 hadi asilimia 40.5, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 na mikakati ya kukuza usawa wa kijinsia nchini.
Katika kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kuhamasisha uundaji na uendeshaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kuanzia ngazi ya vijiji, mitaa, kata, wilaya hadi mikoa, ambapo kuanzia mwaka 2020 hadi sasa, majukwaa 15,147 yameanzishwa na kufikia jumla ya majukwaa 20,748.
Amefafanua kuwa majukwaa hayo yanalenga kuwajengea wanawake uelewa wa masuala ya ujasiriamali, elimu ya fedha, uwekezaji, kutambua fursa, kubadilishana uzoefu wa kibiashara pamoja na kutoa elimu ya malezi bora kwa watoto na vijana.
Kuhusu mashirika yasiyo ya kiserikali, Dkt. Gwajima amesema Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na sera za Taifa, ikiwemo Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 na Mwongozo wa Uratibu wa Mashirika hayo wa mwaka 2003, kwa lengo la kuhakikisha yanachangia maendeleo ya jamii na uwajibikaji wa kijamii.
Ameongeza kuwa Serikali imeboresha huduma za usajili wa mashirika hayo kupitia mfumo wa kidigitali unaojumuisha ramani ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, sambamba na kuanzisha Dawati la Uratibu wa shughuli za mashirika hayo ndani ya Wizara za Kisekta na Sekta Binafsi ili kuimarisha ushirikiano na utoaji wa huduma.
Kupitia miradi inayotekelezwa na mashirika hayo, amesema kuwa jumla ya ajira 8,000 zilitengenezwa kwa mwaka 2008 pekee, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa jamii.
Akizungumzia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Awamu ya Pili, Waziri huyo amesema Serikali imekuwa ikiendesha majadiliano ya mila na desturi katika jamii kwa lengo la kubadili mitazamo hasi kuhusu malezi na makuzi ya vijana, ambapo wasichana 8,956 na wavulana 6,994 walifikiwa kati ya Julai hadi Septemba 2023.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Ajenda ya Taifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025, huku tathmini ya utekelezaji ikipangwa kufanyika mwaka 2026, na kutoa wito kwa vijana kupima afya zao ikiwemo magonjwa ya zinaa na virusi vya UKIMWI.
Kuhusu uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Dkt. Gwajima amesema Serikali inaendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki ya NMB kwa wafanyabiashara wadogo mmoja mmoja kwa riba ya asilimia saba, ikiwemo waendesha bodaboda, bajaji, wachuuzi, washonaji, wasusi, wauza mbogamboga, mama lishe na baba lishe.
Amesema hadi sasa wafanyabiashara wadogondogo 187,000 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 9.9, huku zaidi ya wafanyabiashara 100,000 wakiwa tayari wamesajiliwa kwenye mfumo wa kidigitali wa usajili kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri zao.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (Women Development Fund), ambapo katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2025, wanawake wajasiriamali 45 wamewezeshwa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 337.9.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment