" SERIKALI YAIMARISHA FURSA ZA MAKUNDI MAALUM IKIWEMO WANAWAKE, VIJANA, WATOTO NA WAZEE

SERIKALI YAIMARISHA FURSA ZA MAKUNDI MAALUM IKIWEMO WANAWAKE, VIJANA, WATOTO NA WAZEE



Na Sophia Kingimali

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Serikali inaendelea kutekeleza kwa kasi shughuli za maendeleo na kutoa fursa mbalimbali kwa makundi maalum ikiwemo wanawake, vijana, watoto, wazee na wafanyabiashara ndogondogo katika mwaka wa fedha 2025/26.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Dkt. Gwajima amesema jitihada hizo zinafanyika chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kujenga Taifa jumuishi lenye haki, usawa na ustawi kwa wananchi wote.

Aidha, ameeleza kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inalenga kuwekeza zaidi katika sekta zinazotoa ajira kwa wingi zikiwemo kilimo, utalii, viwanda, ujenzi, michezo, sanaa za ubunifu na madini, hatua itakayoongeza fursa za kiuchumi kwa makundi maalum.

Sambamba na hayo, Waziri huyo amewahamasisha wananchi kutumia vyuo vya maendeleo ya jamii vilivyopo maeneo mbalimbali nchini pamoja na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ili kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri, kuajiriwa na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Katika eneo la malezi ya watoto, amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kupitia Mwongozo wa Wajibu wa Wazazi na Walezi, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa baba na mama katika kumlea mtoto ili kufikia ukuaji timilifu kimwili, kiakili na kisaikolojia.

“Utekelezaji wa Programu ya Furaha Teen katika mikoa ya Songwe na Mbeya unaendelea, programu inayolenga kuwajengea uwezo wazazi katika malezi ya vijana balehe, pamoja na kuwasihi wazazi kuwasikiliza na kuwashirikisha vijana katika masuala ya kifamilia na kijamii,” amesema.

Akizungumzia usawa wa kijinsia, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanawake kushiriki katika nafasi za maamuzi na uongozi, hatua iliyochangia ongezeko la idadi ya wabunge wanawake kutoka asilimia 37.5 hadi 40.5 mwaka 2025.

Kuhusu ustawi wa wazee, amesema Serikali imeendelea kutoa huduma za matunzo, bima ya afya na vitambulisho vya matibabu bila malipo kwa zaidi ya wazee milioni 1.2, pamoja na kuimarisha makazi ya wazee yanayomilikiwa na Serikali na binafsi.

Aliongeza kuwa hadi mwaka 2025, jumla ya Mabaraza ya Wazee zaidi ya 20,000 yameanzishwa nchini ili kuwawezesha wazee kutoa maoni na ushauri katika masuala ya kijamii, pamoja na kurithisha jamii maadili na mila chanya.

Akizungumza kuhusu kulinda haki za watoto, amesema Serikali imeendelea kusajili makao ya watoto na vituo vya kulelea watoto mchana, pamoja na kuimarisha huduma za malezi ya kambo na kuasili, ambapo idadi ya watoto waliopata huduma hizo imeongezeka kutoka watoto 85 mwaka 2022 hadi 562 mwaka 2025.

Aidha, Waziri huyo amesema Serikali inaendelea kupambana na vitendo vya ukatili kupitia kampeni za kijamii na mafunzo kwa wataalamu wa sekta mbalimbali, ambapo mamia ya matukio yameripotiwa na kushughulikiwa ili kulinda makundi hatarishi.

Katika uwezeshaji wa kiuchumi, Dkt. Gwajima amesema Serikali imetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo na wanawake wajasiriamali kupitia Benki ya NMB na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, huku zaidi ya Sh bilioni 9.9 zikitolewa kwa maelfu ya wanufaika.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuratibu mashirika yasiyo ya kiserikali na kuimarisha ushirikiano nao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akitoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kulinda amani na kuzingatia maadili ili kufanikisha maendeleo jumuishi na endelevu.  



Post a Comment

Previous Post Next Post