Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.Uhaba wa malighafi katika viwanda vya kuchakata na kusindika samaki mkoani Kagera umetajwa kuwa changamoto kubwa inayosababisha viwanda hivyo kufanya kazi chini ya uwezo wake halisi, hali inayokwamisha uzalishaji na mchango wake katika uchumi wa mkoa.Hayo yameelezwa na Meneja Usafirishaji wa Kiwanda cha Kuchakata na Kusindika Samaki cha Pride of Nile Pvt Ltd, Melchiad Kezilahabi, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kiwanda hicho kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally, alipofanya ziara kiwandani hapo Izigo, wilayani Muleba, Desemba 29, 2025.Kezilahabi amesema kuwa licha ya kiwanda hicho kuwa na uwezo wa kusindika tani 15 hadi 20 za samaki kwa siku, kwa sasa huzalisha kati ya tani 5 hadi 7 pekee kutokana na upungufu mkubwa wa malighafi.Amebainisha kuwa chanzo kikuu cha uhaba huo ni kuendelea kuwepo kwa vitendo vya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, ikiwemo uvuvi wa dagaa kwa kutumia mionzi ya jua pamoja na biashara holela ya samaki wachanga (changa) mitaani, hali inayopunguza upatikanaji wa samaki wanaokidhi vigezo vya viwandani.Aidha, Kezilahabi ameongeza kuwa kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto ya kibali cha kusafirisha mabondo mabichi kwenda mkoani Mwanza, ambapo hutozwa shilingi 2,000 kwa kila kilo, hatua ambayo inaongeza gharama za uzalishaji.Akizungumza kuhusu mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizo, Kezilahabi amesema kuwa udhibiti madhubuti wa uvuvi haramu utaongeza upatikanaji wa samaki wenye viwango vinavyokubalika. Pia amependekeza Serikali kuchukua hatua za kuhakikisha mabondo yanatumbuliwa rasmi viwandani pindi samaki wanapofikishwa, jambo litakalosaidia kudhibiti biashara haramu ya samaki wachanga."Tunapendekeza kwamba Serikali ichukue hatua za kuhakikisha Mabondo yanatumbuliwa kutoka kwenye samaki wanapofikishwa Viwandani hii itasaidia udhibiti wa mabondo kudhibiti biashara haramu ya samaki wachanga,hatua kali zilizofanywa na wenzetu Uganda na Kenya kwa kuweka Adhabu kali kwa viwanda vya mabondo kwa kuwataka kutumbua samaki katika maeneo rasmi zimetoa matokeo chanya" Amesema KezilahabiKwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally, amekemea vikali tabia ya baadhi ya wasimamizi wa sekta ya uvuvi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa badala ya kulinda rasilimali za taifa.Dkt. Bashiru amesema baadhi ya watendaji wamekuwa wakigeuza mamlaka yao kuwa chanzo cha kujipatia fedha kwa kuwatoza waovu faini zisizo rasmi badala ya kuwafikisha mahakamani, hali inayochochea kuendelea kwa uvuvi haramu.“Badala ya kuhifadhi rasilimali za samaki, baadhi yao wanazihujumu kwa mtindo wa rushwa. Mtekelezaji anapomkamata mhalifu, anajifanya yeye ni mahakama na kumtaja kiwango cha faini, hali inayomlazimisha mhalifu kuchagua ‘unafuu’ badala ya haki,” amesema Waziri Dkt Bashiru.Aidha, Waziri huyo amepiga marufuku viwanda vya kuchakata samaki kuingiza mitumbwi yao majini kwa ajili ya kuvua au kununua samaki moja kwa moja kutoka kwa wavuvi, akisisitiza kuwa hatua hiyo huvuruga soko la uvuvi, huwafilisi wavuvi wadogo na kuwafanya kuendelea kuwa masikini.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






Post a Comment